Na Saleh Ally
MASHABIKI wa soka wa timu kubwa za Ulaya wanafanana mambo kadhaa na wale wa hapa nyumbani Tanzania lakini lazima kuna tofauti.
Moja ya tofauti kubwa ya mashabiki wa timu kubwa hasa za barani Ulaya ni subira na uelewa wa mambo kuhusiana na mchezo wa soka hasa kuhusiana na matokeo yake.
Kwamba inaweza kutokea mkashinda, sare au kufungwa licha ya kwamba mashabiki wa soka “wanajipenda wenyewe tu”, yaani wanataka timu yao ishinde.
Pamoja na kuwa wamekuwa wavumilivu, mara kadhaa wamekuwa wakiwapa deni kubwa wachezaji wao si kwa maneno ya kejeli, badala yake wanaanza kwa kuonyesha wanawaamini na wanajua watafanya vema.
Kawaida wanachopenda wao ni kuwapa deni wachezaji wao ili wajitume zaidi. Wanajua wakiwa pamoja nao na kuwaonyesha wanawaamini, watapambana kweli na ndio maana wanajitokeza viwanjani kwa wingi kuwaunga mkono wakati wakipambana.
Wachezaji wengi wanaocheza katika nchi mbalimbali barani Ulaya, hasa katika ligi zenye ushindani, wanajua ugumu wa mambo na hali ilivyo.
Wanajua maana ya deni la mashabiki, deni la kuepuka kuwaangusha wanaowaamini, ndio maana wanapambana kila dakika 90 kuzifanya ziwe “zao” kwa maana ya kuwapa malipo mashabiki wao kutokana na kuwaamini na kuwaunga mkono kwa nguvu zote.
Bila shaka hii hali ndiyo aliyonayo Mtanzania, Mbwana Samatta ambaye ndiye tegemeo namba moja katika ushambulizi kwenye kikosi cha KRC Genk ambao ni mabingwa wa Ubelgiji.
Samatta amefanya kila analoweza kwa kusaidiana na wenzake, leo Genk imecheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano mikubwa na tajiri zaidi kwa ngazi za klabu kuzidi mabara yote au mikubwa zaidi dunia nzima.
Kucheza hatua hiyo ni fedha na ufahari, ndio maana timu kama Manchester United na Arsenal sasa zinapambana vilivyo kurudisha hadhi yao kwa kurudi na kushiriki tena michuano hiyo lulu.
Samatta ni mgeni Ligi ya Mabingwa Ulaya na ameingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza katika hatua hiyo na kufanikiwa kufunga bao lake la kwanza ikiwa mara ya kwanza katika mechi ambayo KRC Genk walifungwa kwa mabao 6-2 dhidi ya Salzburg.
Deni lake ni kuhakikisha anawaongoza wenzake, nao wanamuongoza ili kuleta angalau ushindi lakini ukiangalia kundi walilonalo ni gumu na linahitaji miujiza wao kuvuka kwenda mbele.
Wapo na mabingwa watetezi Liverpool, wakali kutoka Italia yaani Napoli lakini Salzburg ambao walionekana ni saizi yao kwa aina fulani lakini wameanza kwa kuwavurumisha kwa mabao 6-2.
Sasa watarudi tena katika Ligi ya Mabingwa Ulaya Oktoba 2 wakiwa dhidi ya wababe Napoli ambao kuanza tu, wameitwanga Liverpool kwa mabao 2-0. Vipi KRC Genk? Hakuna ubishi inaogopesha na lazima Genk wanapaswa kujipanga zaidi.
Takwimu walizoanza nazo msimu huu, zinaonyesha kuna ugumu maana katika mechi tatu za ligi, zina uwiano “ulionyooka” maana wameshinda moja, sare moja na kupoteza moja.
Takwimu za namna hii, zipo kwa timu nyingi sana ambazo zinakuwa na maandalizi kwa ajili ya kuanza ligi ya mabingwa. Unaona hata Napoli, katika Serie A, walicheza mechi mbili kabla ya kuivaa Liverpool, wakawa wameshinda moja na kupoteza moja.
Je, KRC Genk wataondoka bila ya pointi hata moja? Maana mechi zijazo ni Napoli, baada ya hapo ni Liverpool, itakuwa Oktoba 23.
Wababe hawa, pamoja na Samatta kuwa na uwezo bora, anaweza vipi kuzivuka ngome za akina Kalidou Koulibaly au Virgil van Dijk?
Anakutana na timu zinazotokea katika ligi zenye ubora zaidi ya ligi anayocheza. Timu zenye wachezaji wa kiwango cha juu na makocha wakubwa kama Jurgen Klopp na mkongwe zaidi Carlo Ancelotti.
Deni la Samatta ni kubwa kuliko alichonacho. Lakini kawaida mwanadamu anaweza kuwa na uwezo mkubwa zaidi kuliko anavyojua na hakuwahi kuutumia.
Yanapotokea matatizo au ulazima wa kuonyesha uwezo huo, anajikuta anakiweza hata ambacho hakukitarajia.
Nani aliamini Samatta angefanya vema zaidi katika kikosi cha TP Mazembe na mwisho kuwa staa? Nani alijua ataipa timu hiyo ubingwa Afrika na pia kufikia hadi kucheza Kombe la Dunia la Klabu? Hakuna haki yetu.
Hiyo ni Afrika, lakini alipokwenda Ulaya hatukumuamini pia, tukaona kuna ugumu sana kwake kwa kuwa Ulaya ni habari nyingine. Mwisho ameipa KRC Genk nafasi ya kushiriki Europa League, msimu uliofuata Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini kabla wamekuwa mabingwa wa Ubelgiji baada ya miaka rundo!
Hivyo huu ndio wakati wa Samatta, kwa kuwa deni lake ni kubwa kuliko alichonacho mfukoni, basi anaweza kujituma zaidi ili kufanya kile ambacho hakutegemea kwa vile dalili zinaonyesha kweli uwezo anao na anaweza kufanya kile ambacho hakikutarajiwa na wengi lakini ni lazima ajiamini, apambane kweli maana haitakuwa kazi nyepesi.
0 COMMENTS:
Post a Comment