ZAHERA ATUMIA DAKIKA 90 KUTENGENEZA MABAO YA BALINYA
Katika kuelekea mchezo wao wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera, juzi Jumamosi alitumia dakika 50 kwa ajili ya kuwapa mbinu za ufungaji mabao washambuliaji wake.
Yanga inatarajiwa kuvaana na Zesco United kati ya Septemba 13 hadi 15, mwaka huu mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo tayari imepoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara iliyocheza wiki iliyopita baada ya kukubali kufungwa na JKT Tanzania bao 1-0, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Zahera alisema nguvu na akili zote amezielekeza kwenye safu ya ushambuliaji ambayo juzi alitumia dakika 50 kwa ajili ya kuwapa program maalum washambuliaji wake, David Molinga ‘Falcao’, Juma Balinya, Sadney Urikhob na Mybin Kalengo. Zahera alisema program hiyo aliifanya kwenye mazoezi ya asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar.
Aliongeza kuwa lengo ni kuona washambuliaji hao wanafunga mabao katika michezo ijayo ya ligi na michuano ya kimataifa wanayoshiriki.
“Bado hakujawa na muunganiko mzuri wa washambuliaji wangu katika kikosi changu hiki kinachojiandaa na mchezo wa Caf dhidi ya Zesco ya Zambia.
“Katika kuhakikisha washambuliaji wangu wanatengeneza muunganiko, nimeona nitumie dakika 50 pekee kwa kuwapa program maalum ya jinsi ya kufunga mabao.
“Ni matarajio yangu kuona washambuliaji wangu wakishika mafunzo na maelekezo yangu ili kuhakikisha wanacheza kwa kuelewana na kufunga mabao mengi,” alisema Zahera.
0 COMMENTS:
Post a Comment