UWANJA wa Nangandwa Sijaona leo mkoani Mtwara, Ndanda FC itaikaribisha Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuwa na ushindani wa kipekee kwa timu zote Ila rekodi za mabao zinaibeba Yanga mbele ya Ndanda.
Ndanda FC tangu ipande daraja msimu wa 2014 haijawahi kuifunga Yanga mabao zaidi ya mawili na katika mechi 10 ambazo wamekutana Yanga imeshinda mechi nne tofauti na Ndanda ambao wameshinda mechi moja pekee na kulazimisha sare tano.
Pia Ndanda imeifunga Yanga jumla ya mabao sita pekee huku Yanga ikiifunga Ndanda mabao 12 kwenye jumla ya mabao 18 ambayo yamepatikana.
Mchezo mmoja tu wa msimu wa 2016-17 ulileta mabao mengi ambapo Yanga ilishinda jumla ya mabao 4-0 Uwanja wa Taifa.
Rekodi za Uwanja wa Nangandwa zinaonyesha kuwa Yanga imefunga mabao mengi kuliko Ndanda kwani kwenye mechi nne ambazo wamekutana Yanga imefunga mabao matatu huku Ndanda ikifunga mabao mawili pekee na kwenye kushinda Yanga imeshinda mara moja na imepoteza mara moja huku ikilazimisha sare mechi mbili.
Mechi moja ya msimu wa 2015/16 haikuchezwa Nangwanda kutokana na makubaliano maalumu ilichezwa Taifa na timu zote zilitoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2.
Kwenye jumla ya mechi hizo 10 Yanga imefunga bao moja tu la penalti iliyofungwa na Kelvin Yondani huku aliyekuwa mchezaji wao wa zamani Amiss Tambwe amekosa penalti mbili hivyo leo moto utawaka kwa timu zote kusaka rekodi mpya.
0 COMMENTS:
Post a Comment