ZUBER Katwila Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar amechaguliwa na kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutwaa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Oktoba.
Jafari Kibaya pia mchezaji wa Mtibwa Sugar amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2019/20
,Mtibwa Sugar ilicheza michezo minne, ikishinda mitatu na kupoteza moja, ambapo iliifunga Ndanda bao 1-0 ugenini mjini Mtwara, ikashinda nyumbani mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania na pia ilishinda nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union na ilifungwa ugenini na Namungo bao 1-0.
Kibaya alikuwa na kiwango kizuri uwanjani kwa mwezi huo akichangia kwa asilimia kubwa mafanikio hayo ya Mtibwa, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili, ambapo aliwashinda Gerald Mathias wa Mwadui na Ditram Nchimbi wa Polisi Tanzania alioingia nao fainali.
Mtibwa ilipanda katika msimamo kutoka nafasi ya 19 mwezi Septemba hadi ya 11 mwishoni mwa Oktoba.
Kama ilivyokuwa kwa Kibaya, Gerald naye alikuwa na kiwango kizuri ikiwa ni pamoja na kufunga katika michezo mitatu kati ya minne ya timu yake, ambapo alifunga bao moja katika ushindi wa Mwadui wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, pia alifunga bao pekee katika mchezo wa Mwadui na Simba, alifunga tena katika mchezo ambao Mwadui ililala mabao 2-1 kwa Coastal Union mjini Tanga.
Mchezo mwingine Mwadui ilifungwa bao 1-0 na Polisi.
Kwa upande wa Nchimbi alionesha kiwango kizuri kwa timu yake, ambapo alifunga hat trick katika mchezo ambao timu hiyo ilitoka sare ya mabao 3-3 na Yanga.
Polisi ilicheza michezo mitano kwa mwezi huo, ambapo licha ya sare ya Yanga, iliifunga Mwadui bao 1-0, ikaifunga Singida United mabao 2-1, ikafungwa na Mtibwa Sugar mabao 2-0 na ikafungwa na Lipuli mabao 2-1.
Kwa upande wa Katwila aliwashinda Mecky Maxime wa Kagera Sugar na Madenge Omary wa Biashara United, ambapo Katwila aliiongoza timu yake katika michezo minne, akishinda mitatu.
0 COMMENTS:
Post a Comment