November 18, 2019



SENZO (KULIA) ALIPONITEMBELEA OFISINI KWANGU GLOBAL GROUP.



Na Saleh Ally
SIKU chache zilizopita ofisini kwetu tulipata ugeni wa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Senzo Mazingisa raia wa Afrika Kusini.


Senzo aliongozana na Mjumbe wa Bodi ya Simba SC, Mulamu Ng’ambi. Lengo ni kutembelea eneo la kazi kama watu ambao tunashirikiana nao kikazi, kuona kazi zetu zinafanyika vipi lakini maandalizi ya habari zetu hadi zinamfikia msomaji, msikilizaji au mtazamaji.


Global tuko nyanja zote kwa maana ya kuwafikia wasomaji kupitia magazeti, wasikilizaji kupitia redio lakini wasikilizaji haohao pamoja na watazamaji kupitia runinga.


Wakati Senzo akiwa katika ofisi zetu, nikiwa na wafanyakazi wenzangu tulipata nafasi ya kumfanyia mahojiano kwa muda wa saa zima hivi. Naye akajiachia na kuchambua mambo vizuri kabisa.


Raia huyo wa Afrika Kusini alinifurahisha sana. Kwanza kwa kuwa aliamua kuwa huru na wazi na kufafanua mambo mengi bila ya uficho. Akaweka wazi kuhusiana na mipango yake lakini hata wachezaji ambao yeye aliamini wana mwendo mzuri wa kwenda katika mafanikio.


Akaeleza wadi mipango yake ya kutowauza baadhi ya wachezaji akiwemo Meddie Kagere na sababu zake zikawa ni za msingi kwa kuwa mauzo hata kama fedha ni nyingi, cha kwanza kuangalia ni timu yenyewe na mwenendo ukoje na kadhalika.


Senzo ni mzoefu katika soka, amewahi kufanya kazi katika klabu kubwa ya Afrika Kusini ya Orlando Pirates lakini baadaye akatua Free State Stars ambayo aliichezea Mtanzania, Mrisho Ngassa katika siku chache ambazo alifanya kazi nchini Afrika Kusini.


Senzo alizungumza mambo mengi sana lakini kati yaliyonivutia ni yake yaliyohusiana na mipango ya muda mrefu na hasa katika suala la kuwaza kuwa Simba kitu cha kwanza kabisa wanatakiwa kufanya ni kuanza kusafisha au kutengeneza nyumba yao na baada ya hapo wataanza kuangalia suala la kukaribisha wageni.


Wanasafishaje nyumba? Senzo anaamini bado nyumba yao haijawa safi kiasi cha kuwakaribisha wageni kwa mbwembwe au uhakika. Hii iko hivi, yaani kabla ya kuanza kukimbilia suala la kutafuta wadhamini kwa ajili ya kuisaidia klabu, kikubwa ni kutengeneza mazingira bora ambayo yataifanya timu iwe inatangazika na kuaminika.


Pale unapokwenda kuomba wadhamini, 
unakuwa na mambo mengi ya kuwaelezea kuhusiana na klabu yako tena vitu unavyovielezea viwe ni vile vinavyotangazika, vinavyowavuta na kuwashawishi wadhamini kulingana na namna ulivyojiandaa.


Kiongozi huyo wa Simba anaona bado hawajawa tayari, wanaweza kupata wadhamini lakini haoni kama watakuwa na uwezo wa kutoa fedha nyingi sana hivyo ameanza na kupambana na ndani ya Simba kabla ya kuanza kukaribisha wageni.


Hakika ninaelewa, lazima Senzo amejifunza mengi katika soka la Afrika Kusini. Vigumu sana watu wengi wanaopenda mpira kujua Afrika Kusini ilivyopiga hatua labda wapate nafasi ya kutembelea nchini humo na kujionea kwa kuwa mpangilio wa mambo yao ni wa kiwango cha juu na ninaweza kusema wamepiga hatua hata kuliko baadhi ya nchi za Ulaya.


Hivyo, Senzo lazima atakuwa tofauti na wadau wengi sana na hasa wenye haraka au mazoea. Kazi yake haiwezi kuwa nyepesi na anapaswa kuungwa mkono na wachache wanaolewa kuendelea kuwaeleza wengi wasioelewa kinachofanyika hakiwezi kukua haraka kama uyoga.


Aliyoyasema Senzo ni mambo nimekuwa nikiyaandika mara nyingi sana hasa baada ya kupata bahati na majaaliwa ya Mwenyezi Mungu kutembelea katika nchi zilizoendelea kisoka kama Hispania, England, Ujerumani, Uturuki na kwingine kwingi.


Huko nikajifunza mengi kupitia katika klabu kama Liverpool, Arsenal, Everton, Manchester United, Real Madrid, Barcelona, Bayern Munich, Borussia Dortmund, FC Kolhn, Galatasaray na nyingine nyingi.


Niliporejea, niliandika na kuzungumzia kuhusiana na yale ambayo nimeyaona. Nikawaeleza viongozi na mashabiki na hata wachezaji. Lakini kumekuwa na kazi ngumu katika kubadilika wengi wakiamini Tanzania ni kama kisiwa na sisi tuna mambo yetu, jambo ambalo ni kujidanganya kwa kiasi cha kuumiza.


Anayoyasema Senzo, mengi mimi nimekuwa shuhuda na niliyaeleza. Lakini hata baadhi ya viongozi wa Simba wakati huo waliona haiwezekani, lakini leo wana nafasi ya kujikumbusha kuwa mtu aliyeajiriwa kwa ajili ya kazi za klabu anawakumbusha mambo yaleyale na yeye ana zaidi kwa kuwa hiyo ndiyo kazi yake.


Vizuri sana kumuunga mkono ili alete asali kwa mpira wetu na mkumbuke kuwa anahitaji watu kumuelewa taratibu na mambo yaende yanabadilika. Kama mtakuwa na haraka, mwisho ataondoka halafu tutaendelea kubaki tulipo.


Ninaona hivi, kama Simba watamvumilia naye akasaidia kupatikana kwa mabadiliko, basi kuna kila sababu ya klabu nyingine za hapa nyumbani nazo kuanza kufuata mabadiliko hayo na huo utakuwa mwanzo wa mabadiliko kwa mpira wetu wa Tanzania ambao wenyewe tumeudumaza kwa muda mrefu tukiamini sisi ni kisiwa.


3 COMMENTS:

  1. Hii habari umejiongelea WEWE ama huyo SENZO... It is too personal...!!

    ReplyDelete
  2. Yanga wanasubiri nini kuiiga Simba katika viwanja walivyopewa kule kigamboni??? Viongozi wao siasa nyingi na kamati za kumwaga....vitendo sifuri....Wawekezaji kama Mo ni vitendo tu. Haya ya kusema wawekezaji ni wananchi kupitia kuchangishana kwenye bakuli na kuuza jezi ni kujidanganya....na ni porojo na siasa....dawa ni kutafuta mwekezaji na aanze vitendo kwa kujenga haraka haitachukua miezi 3 uwanja unatumika wakijenga usiku na mchana

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kama sisi Simba tulivyoiga kwa kitimu cha uchochoroni Gwambina fc ya Mwanza,Yanga jitahidini hata uwe zaidi ya ule wa Azam.

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic