November 8, 2019


INAWEZEKANA kabisa kuwa vile viazi vilivyokatwa katwa na kukaangwa kwenye mafuta vinawalevya wachezaji wetu! Ndiyo hapa nazungumzia chips, chakula pendwa cha watu wengi. Ukila zile unaonekana wa ‘mjini’ au una fedha kiasi hata kama utakula kavu.

Ndoto za wachezaji wengi ni kucheza soka la kulipwa, ndiyo hiyo ni dunia nzima, kule Amerika wanawaza kwenda kucheza Ulaya hata Afrika wanawaza kwenda huko, kwa kifupi wengi wanapenda kwenda kucheza sehemu ambayo wataifurahia.

Sasa hapa kwetu, wachezaji wetu wengi wanapenda sana kucheza Yanga na Simba, hizi ndizo klabu kongwe na maarufu hapa Bongo.

Hata kama zitakuwa na hali mbaya kiuchumi na wakaletewa ofa ambayo ni ndogo tofauti na ile watakayoleta Azam au Mtibwa mchezaji hapindui kucheza kwa kulwa na doto, hizi ndizo ndoto zao.

Anaona wazi pale hakuna nafasi ya kucheza wala hajali atang’ang’ania hapohapo, hii yote anataka akacheze hapo, hajali kesho yake wala kipaji chake.

Sasa wanapojiunga na timu hizo kongwe akacheza mechi moja na kufanikiwa kuwateka mashabiki ndiyo basi tena ataanza kwenda kujirusha na yeye.

Utamwambia nini sasa ameshakubalika na mashabiki kwa mechi moja tu, hapo kama alikuwa analala saa 3 usiku basi ratiba itabadilika ataanza kukesha kule wanakopiga Wazee wa Ngwasuma, Twanga Pepeta au Sinza kwenye vibanda vya chips.

Chips za Dar ni tamuuu hasa Sinza na mitaa fulani sasa hapo akili yote inahama, huko kuna vishawishi kadhaa na mchezaji asipokuwa makini basi anapotea kabisa huyo mchezaji.
Kucheza Dar tena Yanga au Simba na ukafanikiwa kuteka watu basi baada ya hapo inahitaji uvumilivu na kuamini zaidi katika ndoto zako ili kuweza kukifanya kile ambacho kimekupeleka hapo.

Tanzania tuna uhitaji mkubwa sana wa wachezaji wa kwenda kucheza nje na kuongeza uzoefu wa mechi kubwa.

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayecheza Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji alishasema ni vyema wachezaji wetu wengi wakatafuta nafasi ya kwenda nje kuongeza uzoefu sasa ni wakati wenu, tumieni teknolojia iliyopo kujiuza.

Siku hizi mambo yamerahisishwa, unafungua akaunti yako Youtube unaomba video zao pale Azam Media wanakupa unatupia zingine unasambaza kwenye klabu mbalimbali duniani, sasa kama una kipaji utafanikiwa tu hata kama itakuwa kwa kuchelewa. Yaani kama ipo ipo tuuu.

Ukishachukulia mpira kama nidyo kazi yako rasmi lazima utafuata ile misingi ya kuhakikisha unafanikiwa na kufika mbali zaidi.

Haiwezekani wewe kila siku ukihojiwa na Waandishi wa Habari unasema unataka kwenda kucheza soka nje ya nchi sasa mbona huendi na uwezo wa kucheza unao.
Tuliona TP Mazembe walitua kwa Ibrahim Ajibu lakini dili likaisha juu juu tena wakati huo kijana alikuwa moto sana, sasa nafasi kama hizi kwa nini hamzitumii vizuri zikija. Au chips za Sinza zinawafanya mshindwe kufikiria nje ya boksi?

Huko TP Mazembe ndiko alikopita Samatta na amekuwa ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wa Tanzania kutokana na uvumilivu na nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja jambo ambalo kimsingi limemjenga na kumfikisha hapo alipo sasa.

Safari ya kuelekea mafanikio kama aliyokuwa nayo Samatta, inahitaji moyo wa uvumilivu, nidhamu na kutokubali kurudi nyuma, hata kama safari hiyo ina vigingi na miba ndani yake.

Wengi walijaribu lakini mwisho wa siku tumekuwa tukishuhudia wakirudi kimya kimya na visingizio lundo. Tamaa ya mafanikio itamsaidia kila mmoja kufikia malengo yake na kutimiza ndoto yake.  

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic