January 27, 2020


BONDIA wa zamani hapa nchini Rashid Matumla ‘Snake Boy ‘ameweka wazi kuwa anatamani kuhamia Mkoa wa Manyara ili kuweza kuwanoa vizuri vijana wa mkoa huo wanaojihusisha na mchezo wa ngumi.

Matumla ameyasema hayo wakati wa makabidhiano ya ulingo wa ngumi wa kisasa iliyogharimu shilingi milioni 4 ambao ulitolewa na mdau wa mchezo huo mikoa ya Arusha na Manyara ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya COTECH Developers Limited, Mhandisi John Kahembe kwa lengo la kufufua mchezo huo mkoani Manyara hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Kwaraa mjini Babati.

Matumla amesema Manyara wamejitahidi sana kuwa na ulingo wa kisasa kwani mchezo huo unahitaji ulingo kwa ajili ya kufanyia mazoezi ya kila siku lakini pia kwa ajili ya kujitengenezea uwezo mkubwa wa kufanya mashindano ndani na nje ya nchi.

“Ulingo ndiyo kila kitu kwa sababu siku zote ukiona watu wanacheza Marekani pamoja na nchi zingine wanafanikiwa ujue unacheza kwenye ulingo, kama mkoa unakosa ulingo kwa kweli inakuwa hamna kitu lakini wachezaji wanapata hamasa kutokana na ulingo kuwepo na watafanya vizuri.

“Mimi mwenyewe nimeomba kuishi hapa, kama nitapata nafasi hii ya kuishi hapa nitazidi kuwabeba juu, nimependa hali ya hewa ya Manyara kama mambo yataenda vizuri basi tunaweza kuwa pamoja na nikazidi kuwaendeleza vijana,’’ alisema Matumla.

Amesema kuwa lengo la kutaka kuhamia Manyara ni ni kwa ajili ya kukuza vipaji kwani ameona mkoa huo wana uwezo mkubwa katika mchezo wa ngumi lakini wanakosa sapoti ya waalimu wazuri ambao wanaweza kuwafanya kuwa bora na kujitangaza ndani na nje ya Tanzania.


“Dar es Salaam wacheza ngumi ni wengi na ni maarufu, mimi nimeamua kuja kukaa Manyara ili tuendeleze mchezo huu vizuri endapo tutakubaliana,” alisema Matumla.

Kwa upande wake madau wa mchezo wa ngumi mikoa ya Manyara na Arusha ambaye pia ni mmiliki na mwanzilishi wa Kampuni ya Cotech Developers Limited, mhandisi Kahembe amesema ni wakati wa wadau mbalimbali mkoani hapo kujitoa kwa ajili ya kuwasaidia vijana ambao wana malengo kupitia michezo kwani huko wanaweza kupatikana mabilionea wengi.


Amesema Wanamanyara inatakiwa wajitahidi kuwashika mikono vijana wao pale wanapoona wana kitu kikubwa kwa ajili ya kunyanyua uchumi wa nchi, kwani wanaweza kutengeneza matajiri wazuri wa nchi wengi endapo tu watawasaidia hao vijana ambao wanavipaji vikubwa lakini wanakosa mahitaji mbalimbali ya kuwafanya watekeleze majukumu yao vizuri ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Afisa Michezo wa Mkoa wa Manyara, Charles Maguzu amesema mkoa huo hawatakuwa wachoyo wa kuwaazima mikoa ya jirani ulingo huo, kwani lengo ni kukuza vipaji vya ndani ya nchi ili taifa kwa jumla liweze kupata wachezaji wengi ambao wataliletea heshima taifa pale watakapoliwakilisha nje na ndani ya nchi.

Hafla hiyo pia ilisindikizwa na mapambano ya wazi kutoka mabondia kwa mikoa ya Arusha, Singida, Mwanza na Manyara ambapo katika matokeo ya jumla mabondia wa Manyara ndiyo waliibuka mabingwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic