MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, raia wa Ghana, Bernard Morrison, amewaondoa hofu Wanayanga kwa kuwaambia kuwa kama lilikuwepo tatizo la ushambuliaji kwenye timu hiyo, basi wakae wakijua limeisha baada ya kutua yeye.
Kauli hiyo aliitoa mshambuliaji huyo hivi karibuni mara baada ya kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo dakika za mwisho kabla ya usajili wa dirisha dogo kufungwa Januari 15, mwaka huu.
Morrison ni kati ya wachezaji sita waliosajiliwa na timu hiyo katika usajili huu wa dirisha dogo, wengine ni Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Muivory Coast, Yikpe Gnamien, Adeyum Saleh, Tariq Seif na Ditram Nchimbi.
Morrison alisema kuwa amekuja Yanga kufanya kazi na siyo kitu kingine, hivyo alichopanga ni kutumia vema kila nafasi atakayoipata kufunga na kutengeneza nafasi kwa wachezaji wenzake, za kufunga mabao.
Morrison alisema kuwa Yanga wamemsajili kwa ajili ya kazi hiyo ambayo ni lazima aifanikishe mara atakapoanza kucheza michezo ijayo, ukiwemo wa Ligi Kuu Bara unaofuata dhidi ya Singida United utakaopigwa keshokutwa Jumatano huko Namfua, Singida.
Aliongeza kuwa anafurahi mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa wachezaji wenzake, benchi la ufundi huku akiomba sapoti kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo kwa kipindi chote atakachokuwepo Yanga.
“Viongozi wa Yanga wamenileta hapa kwa ajili ya kazi moja pekee ya kufunga mabao na siyo kitu kingine, hivyo ni lazima nitimize hicho kilichonileta kwa kuhakikisha ninafunga mabao katika timu.
“Kufunga mabao ni sehemu ya wajibu wangu katika timu, hivyo niwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa nitatimiza kile kilichonileta Yanga ambacho ni kuifungia timu yangu mabao.
“Ninaamini hadi viongozi wamefikia hatua ya kunisajili ni baada ya kuona kuna tatizo la ushambuliaji katika timu, ninaamini kama lisingekuwepo hilo basi nisingekuwa hapa, hivyo niahidi kuifungia Yanga mabao,” alisema Morrison aliyewahi kuzichezea Orlando Pirates naMotema Pembe.
0 COMMENTS:
Post a Comment