USAJILI wa Mbwana Samatta kwenda Aston Villa katika timu ambayo inashika nafasi ya 18 kabla ya mechi yao ya juzi Jumamosi, unaweza kuwa sahihi kwake licha ya kwamba timu hiyo ipo kwenye nafasi mbaya na hatari ya kushuka daraja.
Ubaya wa nafasi hiyo haifanyi moja kwa moja kuamini Aston Villa itashuka daraja, uwepo wa Samatta kikosini hapo unaweza kuwa chachu ya kuifanya timu hiyo ikabaki ligi kuu.
Wakati Samatta anatua TP Mazembe mwaka 2011, hakuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, ilimchukua muda kidogo, baadaye ndiyo akawa mchezaji tegemeo kikosini hapo.
Njoo katika kikosi cha KRC Genk, Samatta alitua hapo mwaka 2016 katika usajili wa Januari kama ilivyo sasa, pia hakuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.
Alianza mdogomdogo akicheza dakika kadhaa kwa kupishana na Mgiriki, Nikolaos Karelis, baadaye akawa anacheza mwanzo mwisho baada ya Mgiriki huyo kuondoka.
Kukomaa huko kwa Samatta ndani ya Genk, kukampa nafasi ya kuwa nahodha msaidizi ndani ya kikosi hicho ambacho msimu huu alikiongoza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini timu haikufanya vizuri. Ikaishia hatua ya makundi ikishika nafasi ya mwisho kwenye kundi lake.
Ukifuatilia vizuri ndani ya kikosi cha Aston Villa, utagundua kwamba Samatta ana nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza sana. Kwanza ni pendekezo la kocha wa timu hiyo, Dean Smith, ambaye anataka mshambuliaji wa kuziba nafasi ya Mbrazil, Wesley Moraes ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima kutokana na kupata majeraha.
Kumbuka Moraes alikuwa tegemeo kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo akicheza mechi 21 kati ya 22 za Premier msimu huu na kufunga mabao matano. Mshambuliaji tegemeo aliyebaki baada ya Moraes kuumia, alikuwa Jonathan Kodjia ambaye naye ameelekea Qatar kujiunga na timu ya Al Gharafa.
Jack Grealish ambaye ni kinara wa mabao akiwa nayo nane na asisti sita, yeye anacheza nafasi ya winga, Conor Hourihane mwenye mabao saba na asisti 2, ni kiungo wa kati, Anwar El Ghazi ana mabao sita na asisti sita, yeye pia ni winga.
Hivyo Aston Villa baada ya kuumia kwa Moraes, timu hiyo haina mshambuliaji wa kati halisi wa maana. Washambuliaji waliobaki ni Keinan Davis, yeye amecheza mechi sita, Cameron Archer na Indiana Vassilev, walikuwa bado hawajacheza mechi yoyote ya Premier.
Kocha Smith hana sababu za kumsubirisha benchi Samatta, kilichobaki ni kumuanzisha pale kati, asubirie krosi za kina Grealish na zile pasi za mwisho za Anwar El Ghazi, aweke mpira kambani.
Ukitaka kufahamu ni kwa namna gani Samatta anahitajika zaidi kikosini hapo, ni jinsi klabu hiyo ilikuwa ikihangaika kumtafutia kibali cha kufanya kazi England, walitaka waliwahishe dili hilo ili aweze kucheza mechi ya jana dhidi ya Brighton, lakini ikashindikana.
0 COMMENTS:
Post a Comment