March 15, 2020



KUNA msemo mmoja wa Kiswahili unasema ukikiona cha nini kuna wenzio wanaosema watakipata lini ili waweze kukitumia tena kwa umakini zaidi na faida kubwa kuliko wewe unayekidharau.

Kuna mambo mengi sana kwenye maisha yetu sisi Wabongo tunayachukulia poa tena zaidi ya poa, kumbe bado yana thamani kubwa na msaada tosha kwenye jamii.

Kuna wakati macho yetu yanakuwa magumu kuona kitu au kugundua thamani ya vitu na wanakuja watu kutoka nje ya nchi wanafanya hivyo na kutuacha tukiwa midomo wazi na kushangaa.

Mtu aliyetushangaza zaidi kwenye soka letu ni Kocha wa Yanga, Luc Eymael ambaye amegundua thamani ya mlinzi Said Juma Makapu aliyekosa thamani kabisa kwenye soka letu hapo kabla.

Ni kweli kabisa Makapu hakuwa na hadhi yoyote ndani ya Yanga na soka la Bongo kwa ujumla, lakini hivi sasa ni mlinzi mwenye heshima kubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, yote hiyo ni kwa sababu amekuja mtu aliona kitu ndani yake ambacho sisi hatukukiona.

Ubora wa Makapu umesababishwa na Kocha Luc Eymael na hadi ameitwa timu ya Taifa kwa sababu tu kuna mtu amegundua kitu kizuri ndani yake ambacho tulishindwa kukiona.

Makapu tusamehe sisi maana tulikosea na kukuona ni mchezaji wa kawaida mno kumbe kuna kitu tulikuwa tumekosa kukiona kwako hadi kocha wako amekuja kutuonyesha.

Nani asiyempenda Makapu hivi sasa? Nadhani hakuna kwa sababu amekuwa mlinzi wa kati mwenye ubora wa hali ya juu na mwenye uwezo mkubwa wa kuzuia na kuanzisha mashambulizi.
Angalia muunganiko wake pale kwenye ulinzi wa kati ndani ya Yanga akiwa na Mghana Lamine Moro, lazima ukubali kweli wamepikwa na wakapikika kisawa sawa.

Mimi lazima nikubali nilishamtoa Makapu kwenye orodha ya wachezaji wa Yanga msimu ujao, kumbe kuna mtu aliyekuwa anatushangaa tu kwa mawazo yetu mgando yaliyokosa mtazamo wa mbele zaidi.

Makapu anatupa somo kubwa mno na kwamba kuna mengi ya kujifunza kutokana na hayo yanatokea kwa mlinzi huyo wa kati.

Kuna wachezaji wengi kwenye klabu za ligi kuu na madaraja ya chini tunawaona ni wa kawaida mno na hawana hadhi yoyote hadi kwenda kutafuta wachezaji nje ya nchi kumbe kuna watu wanaweza kuifanya hiyo kazi.

Makocha wengi walimpanga Makapu kwenye sehemu ya kiungo mkabaji, kumbe sehemu yake sahihi ambayo anaiweza kwa kiwango cha hali ya juu ni ulinzi wa kati, siyo kiungo.

Makapu atupe somo kwa sisi tunaojiita watu wa mpira na ambao kazi yake ni wa kuwazodoa wachezaji na kuwashusha hadhi yao kila kukicha kumbe ukiwepo umakini wachezaji haohao bado wanaweza kufanya kitu kizuri kwetu.
Sidhani kama kuna mtu hivi sasa hampendi Makapu na kama yupo basi kwa chuki zake tu lakini ukweli utabaki palepale kuwa jamaa anajua na amerudi tena kivingine.

2 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic