Na Saleh Ally
UGONJWA wa Corona sasa ni tishio la dunia na unaona umelazimisha kusimama hadi kwa michezo mbalimbali duniani ukiwemo ule wenye nguvu zaidi kuliko mingine, soka.
Hata ligi kubwa na maarufu kama Premier League ya England, Bundesliga ya Ujerumani, La Liga ya Hispania, Serie A ya Italia na Ligue 1 ya Ufaransa nazo zimesimama.
Ligi Kuu Tanzania Bara nayo imesimama, kwa kifupi hakuna mwenye nguvu ya Corona na wachezaji wanalazimika kubaki nyumbani na kufanya mazoezi wakiwa huko.
Bernard Morrison ni mshambuliaji mpya wa Yanga ambaye amejiunga na klabu hiyo kongwe nchini akitokea kwao Ghana.
Kutokana na tatizo hilo la Corona, Morrison ambaye anaishi na ndugu zake jijini Dar es Salaam amelazimika kuendelea kujifua akiwa nyumbani ili kujiweka fiti.
Amekuwa akifanya mazoezi katika eneo la nyumba anayoishi Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na anasema lengo ni kuhakikisha anahifadhi kiwango.
Morrison anakiri, mambo yamebadilika na hakuna ujanja, analazimika kuwa hivyo kwa kuwa suala la usalama ni muhimu.
MAZOEZI:
Umekuwa ukifanya mazoezi nyumbani, unafikiri yanaweza kukusaidia kuhifadhi kiwango chako?
Nimekuwa nikifanya mazoezi na ndugu zangu hapa nyumbani, lengo ni kuhifadhi kiwango changu kwa kuwa kama unavyoona kwa sasa si wakati mzuri sana kutokana na ugonjwa wa Corona kuishambulia dunia karibu kila sehemu, hali inayotulazimisha kukaa nyumbani kwa ajili ya usalama.
Najitahidi kufanya mara mbili kwa siku, kwanza asubuhi na baadaye jioni saa 11 au 12, tunafanya mazoezi mepesi. Mchana tunaendelea kubaki ndani hapa tukicheza michezo mbalimbali na kufurahi pamoja lakini pia kupumzika.
Unajua kipindi hauna mazoezi, unaweza kujikuta umeongezeka uzito kabla ya ligi kuanza. Hivyo ninajitahidi sana kuwa fiti kwa kiwango hiki.
Suala la kuthibiti chakula ni muhimu, tunahitaji sana kupata chakula ambacho hakiwezi kusababisha uzito kupanda. Kufanya mazoezi na timu na hivi nyumbani kuna utofauti mkubwa. Hivyo tunaweza kubadili aina ya vyakula kwa wakati huu na hofu ni hiyo, kutoongezeka uzito maana ikiwa hivyo, kurudi katika kiwango sahihi inakuwa shida sana.
MWAKA BILA KUCHEZA:
Ulikaa mwaka mzima bila ya kucheza, vipi ukaweza kuanza na kuwa fiti baada ya muda ulipotua Yanga?
Nilikuwa najiandaa tayari kama nitasajiliwa na timu, sikuwa ninakaa tu. Nilikuwa nikipata baadhi ya ofa na nilijua kuna siku moja nitakwenda kucheza.
Nilijua pia kokote ntakaposajiliwa katika kipindi kile lazima nitakuta ligi inaendelea, hivyo niliendelea na mazoezi kuhakikisha siwaangushi watakaonisajili.
Baada ya kusajiliwa na Yanga unaona, nilipofika baada ya siku tatu tu nilitakiwa kucheza mechi yangu ya kwanza na uliona namna ilivyokuwa. Hii ilitokana na maandalizi ambayo nilikuwa nikifanya mara kwa mara kujiweka imara, hivyo niseme mazoezi yalinisaidia sana kabla sijaja.
LIGI YA TANZANIA:
Umecheza mechi kadhaa za Ligi Kuu Bara, unaionaje ligi na unaweza kuitofautisha au kuifananisha vipi na ligi za nchi ulizocheza kabla?
Mfano ni Afrika Kusini, wao wana viwanja bora kabisa kwa maana ya sehemu ya kuchezea lakini viwanja vizuri sehemu ya kukaa na kadhalika. Hauwezi kufananisha na Tanzania au Ghana au Congo ambako nimecheza pia.
Bado ninaamini kuna muda wa kujirekebisha na Tanzania wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi ya hapa hasa katika suala la kurekebisha viwanja vyao na kuvifanya kuwa na ubora sahihi ili kuboresha kiwango cha uchezaji na kiwango cha ubora wa soka la Tanzania kwa ujumla.
Pamoja na hivyo, hapa mashabiki kwa kweli sijawahi kuona katika maisha yangu yote ya kucheza. Mashabiki wa hapa wanawapenda sana wachezaji wao, wako tayari kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwaunga mkono wachezaji wao ili wafanye vema.
Namna mashabiki wa Tanzania wanavyozipokea timu zao uwanjani na kuziunga mkono, kwangu sijawahi kuona na hii inakufanya mchezaji kucheza kwa juhudi kubwa kwa hofu ya kutowaangusha mashabiki wako ambao wanaonekana wako tayari kwa ajili yako na wenzako.
0 COMMENTS:
Post a Comment