April 12, 2020


AZAM FC ni miongoni mwa timu ambazo zinazidi kufukuzia mafanikio ambayo zinayafikiria kila siku iitwapo leo jambo ambalo linazidi kufungua njia kwa wengi kujifunza kwao.
Kwa sasa Ligi Kuu Bara ikiwa imesimamishwa kutokana na kusambaa kwa Virusi vya Corona tunaona kwamba bado Azam FC wamekuwa ni mabalozi wazuri kwa jamii kuhusu kujikinga na kuchukua tahadhari ya Virusi vya Corona.
Wamekuwa wakifanya hivyo kupitia kurasa zao rasmi za Istagram pamoja na ziara za viongozi wao kwenye vyombo vya habari wakijaribu kueleza namna ambavyo wanafanya kuchukua tahadhari na kuwaomba mashabiki pia kuwa mabalozi wazuri.
Nilipata bahati ya kuzungumza na Ofisa Habari aliyechukua mikoba ya Japhary Maganga Zaka Zakazi alipotembelea Ofisi za Global Group hivi karibuni aliniambia kwamba kuna mipango mingi ya kufanya ila cha kwanza ni afya za mashabiki na wachezaji.
Mbali na hayo mengi tulizungumza kuhusu namna ambavyo Azam FC imejipanga kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa kwa kuanza na uwekezaji makini pamoja na kuwa na wachezaji bora.
Katika hilo Azam FC imefungua njia na upande wa kuwa chuo cha kutengeneza wachezaji ni miongoni mwa timu hapa Bongo ambazo zinatengeneza wachezaji wazuri na wanaofanya makubwa kwenye Taifa.
Kwenye anga za kutengeneza wachezaji wanakula sahani moja na Mtibwa Sugar ambao nao wapo vizuri kwenye kutengeneza wachezaji ambao wanakuja kuwa tegemeo hapo baadaye.
Tunaona wachezaji  kama Erasto Nyoni, John Bocco,Gadiel Michael, Metacha Mnata hawa wamepitia Azam FC na sasa wanategemewa ndani ya timu zao pamoja na timu ya Taifa hili ni jambo la msingi.
Pia ukiachana na uwekezaji kwa wachezaji Azam FC imejikita kwenye kuboresha mazingira ya miundombinu ya wachezaji ambapo kila siku yanaboreshwa hapa kuna kitu ambacho klabu nyingine zinapaswa zijifunze.
Haina maana klabu nyingine hazifanya hapana ila nazungumzia utofauti wa maisha ambayo wanapitia vijana wanaoishi pale Azam FC pamoja na vijana wanaoishi sehemu nyingine.
Imekuwa ni rahisi kwa Azam FC kuwaruhusu wachezaji ambao hawana namba ya kudumu ndani ya kikosi kwenda kucheza sehemu nyingine kwa mkopo na kisha baadaye kuwauza jumlajumla.
Tunaona mfano mzuri kwa Ditram Nchimbi walimchomoa huyu jamaa pale Njombe Mji kisha akashindwa kufiti kikosi cha kwanza wakampeleka Mwadui FC kisha baadaye Polisi Tanzania na sasa wamemuuza Yanga.
Ukiachana na Nchimbi pia yupo Andrew Simchimba ambaye yeye alikuwa akikipiga Coastal Union kwa mkopo alipoiva wamemrudisha kikosini anaendelea na maisha yake akiwa na uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza.
Pia uwanja wao ambao wanaufanyia marekebisho ni sehemu ya maendeleo yao jambo linalowafanya wazidi kuwa bora ndani ya Afrika Mashariki na kati wanaonyesha kwamba wamekuja kuwekeza kwenye soka la ushindani.
Ifike wakati na klabu nyingine kutazama namna gani zinaweza kuwa zinatengeneza wachezaji wao na kuwatumia kuwa mtaji hapo baadaye hii itasaidia kupunguza gharama za usajili na badala yake mtaji wa kwanza unakuwa upo mikononi mwao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic