May 29, 2020




NA SALEH ALLY
NAJUA limekuwa ni suala ambalo linazungumzwa mara kwa mara kuzishauri timu kuwa na viwanja vyao binafsi.

Jambo hili tumelizungumza sana kama wadau wa michezo lengo likiwa ni kuzishawishi timu kumiliki viwanja kwa ajili ya maendeleo.


Mara kadhaa wakati wa mjadala wa hili suala, wakati mwingine imekuwa ikionekana ni kama kuzisakama timu hizo.


Maana kila unaposema ni hasara au haifai kwa klabu zikiwemo zile kongwe kutokuwa na viwanja vya mazoezi, ndiyo hapo utasikia wewe ni Yanga au wewe ni Simba tuachie timu yetu.


Najua, leo unaona klabu kama Simba ina viwanja vyake vya mazoezi na unaona namna mashabiki wanavyojivunia lakini unawaona namna baadhi ya viongozi wanavyoonekana kuwa mashujaa kwa kufanikisha jambo hilo.


Hakuna hata mmoja uliwahi kumsikia akisema tunawapongea wadau au wanahabari kwa kufanya kazi nzuri ya kuhamasisha miaka nenda rudi kuwashawishi viongozi kupambana hadi leo tumekuwa na viwanja vya mazoezi.


Utasikia wanapongezwa hadi wale ambao hawakuhusika au wamehusika mwishoni tena kidogo sana. Jambo ambalo ninaweza kusema haliwezi kuwa kitu kinachokwaza, na nimesema hivi kwa ajili ya kukumbusha tu.


Kilichonifanya kukumbuka suala la viwanja leo ni hali hii ya mapambano dhidi ya maambukizi ya Corona. Maisha yamebadilika kabisa na mambo yanakwenda tofauti na namna tulivyozoea.


Hali imekuwa hivi; si hapa nyumbani Tanzania pekee lakini karibu kila sehemu duniani kwa kuwa aina ya maisha imebadilika kutokana na kila upande watu kuishi kwa kutaka kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya Corona.


Kutokana na hali hiyo unaona kuna vitu kadhaa vya maisha ya kawaida ambavyo huenda hatukufikiria kama siku moja kama leo vingebadilika. Mfano kupeana mikono au kukumbatiana wakati wa kusalimiana au kusogeleana. Yote haya ni mambo ambayo hayawezekani katika kipindi hiki.


Hali hii ipo hata katika mchezo wa soka, unaona leo mpira kuchezwa bila ya mashabiki ndiyo jambo sahihi na linalotakiwa.

Wakati kabla ya hapo, ukiamriwa kucheza bila ya mashabiki, maana yake unaadhibiwa kwa jambo fulani kwa kuwa inaumiza kichumi lakini hata kisaikolojia ya uhalisia ya mchezo wa soka.


Sasa unaona, taratibu hali inaanza kurejea katika mstari, timu zinaanza kurudi mazoezini na ligi zimeanza kuchezwa sehemu kadhaa.


Hapa nyumbani, unaona juzi Yanga walifanya vipimo vya afya baada ya kukutana jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza mazoezi, hali kadhalika Simba pia nao waliingia kambini rasmi wakiwa wamepanga kuanza rasmi mazoezi juzi kujiandaa na Ligi Kuu Bara ambayo tayari serikali imeruhusu irejee na kinachosubiriwa ni ratiba tu.


Hapa ndipo kuna somo jingine, huenda utakuwa vizuri kabisa kuzitumia hizi timu kubwa na maarufu zaidi katika Ligi Kuu Bara. Yaani Simba, Yanga na Azam FC.


Kipindi hiki cha maambukizi, maana yake kila timu inapaswa kuwa makini kuhakikisha hakuna maambukizi yanayopatikana katika kikosi chake ili kufanikisha kumalizika kwa ligi.


Azam FC wanaweza kuwa na mazingira mazuri zaidi ya kufanya mazoezi, wachezaji wakatoka kwenye basi na kuingia mazoezini, baada ya hapo wakarejea hotelini.


Hii pia inaweza kuwa hivyo kwa Simba, ambao kwa sasa wana kambi bora zaidi, wana sehemu yao nzuri zaidi ya kufanyia mazoezi. Hii inaweza kuwa pia kwa baadhi ya timu kama Mtibwa Sugar, timu za majeshi.


Tujiulize kwa timu kama Yanga, leo wanaweza kulichukua somo hili tena kwa wakati mwingine kama kitu kibaya kwa timu ya Kariba yao kutokuwa na uwanja wa mazoezi.


Kupanga mabadiliko ya katiba, kupanga usajili bora na mengine ni jambo zuri lakini bila ya kuwa na uwanja wa mazoezi, ni tatizo kubwa na lazima kulifanyia kazi.


Mliopo Yanga, msione mnafanya makubwa sana, vizuri mkafanya yaliyo ya muhimu hata kama hayana sifa kubwa kwa jamii, yanakuwa na maana kubwa katika maendeleo kwa miaka mingi zaidi.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic