WAANDISHI wa Habari Walioa wamepoteza kwa kufungwa kwa penalti 4-1 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Wasioa uliochezwa leo Uwanja wa Chuo cha Sheria Ubungo baada ya dakika 90 kukamilika kwa sare ya kufungana mabao 2-2.
Ibrahim Mohamed aliwatanguliza walioa kwa mabao yake mawili ya kipindi cha kwanza, kabla ya Abdulghafary Ally mwandishi wa gazeti la Championi alisawazisha bao moja kipindi hichohicho cha kwanza.
Juma Ayo alifunga bao la pili kwa wasioa kipindi cha pili na kufanya ubao usomeke 2-2 na matokeo yakabaki hivyo hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi wa kati Heri Sasii inapulizwa.
Baada ya ushindi huo kocha wa wasioa FC, Wilson Oruma alisema: “Tulikua na kila sababu ya kushinda katika huu mchezo, kwa sababu moja kubwa tu, soka linachezwa na vijana, wazee kazi yao ni kuoga maji ya moto, kwahiyo kazi wanayo watafute kwa kujificha.”
Kwa upande wa kocha wa walioa, Thabit Zakaria, (Zaka za Kazi), alisema: “Tumekubali kufungwa, lakini siku zote penati hazina mwenyewe, tulishawaweza hawa wahuni sema ndiyo hivyo tulikosa umakini katika kumalizia nafasi tulizotengeneza, kwa sababu mpira wenyewe tumecheza sisi.”
Mchezo huo ambao ulikuwa na lengo la kuipokea tarehe ya kurejea kwa michezo Juni Mosi pamoja na kujenga ushirikiano kwa waandishi wa michezo nchini.
Ulihudhuriwa na viongozi wengi kama vile Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau, Mkurugenzi wa Michezo na Oscar Mirambo.
Wengine ni Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, Mwenyekiti wa zamani wa Simba ambaye pia alidhamini mchezo huo, Sued Mkwabi, meneja wa zamani wa Yanga, Hafidh Saleh na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara ambaye alikuwa timu wasioa na ulihudhuriwa na mashabiki wa kutosha.
Mshindi alikabidhiwa kombe lililotolewa na Shafih Dauda na kisha kukata keki. Waamuzi wenye beji ya Fifa waliamua mchezo huo Heri Sasii, Soud Lila na Frank Komba, huku watu wa msalaba mwekundu wakilinda usalama wa wachezaji.
Kaka Saleh Jembe, Heshima yako Mkuu!
ReplyDeleteKwa heshima zote napenda kueleza masikitiko yangu juu ya ninachokiona hapo kwenye hiyo VIDEO ya mechi ya Waandishi wa Habari. Hawa ndio waelimishaji wakuu na kioo cha jamii katika mambo mbalimbali, hususani kwa wakati huu jambo muhimu likiwa ni elimu ya afya ya jamii kuhusu njia za kawaida sana na rahisi za kujikinga na ugonjwa wa Virusi vya Korona (COVID-19). Ugonjwa huu bado upo duniani, na hivi karibuni tu nchini Korea Kusini baada ya kuruhusu shule zifunguliwe kwa mafungu, walibaini maambukizi mapya kadhaa ya COVID- 19 ndani ya wiki ya kwanza tu ya shule kufunguliwa. Inasikitisha kuona watu wanaotegemewa kuwa na ufahamu mkubwa wa janga hili, wanaonekana kutokuwa makini na wenye tahadhari. Tazama hakuna hata mmoja wao aliyevaa Barakoa, tazama jinsi walivyosogeleana karibu na hatuna uhakika kama wachezaji walipimwa kwa utaratibu wa uhakika wa kiafya. Kulikuwa na haraka gani ya kufanya hii mechi ambayo haina umuhimu wowote na hivyo kuhatarisha afya za wanaoshiriki hapo na familia zao kule majumbani na wengine wengi wanaoweza kuonana nao baadae? Kuna haja ya kujitathmini hapo na kujirekebisha kwa kuitaarifu jamii kwamba ruhusa iliyotolewa na serikali kuhusu kufanya shughuli za michezo haikumaanisha mambo yafanyike kiholela namna ile. Nawasilisha.