KAMA ambavyo kila siku nimekuwa nikisema, Juni Mosi, mwaka huu ndiyo michezo imeruhusiwa kuendelea hapa nchini baada ya kusimamishwa tangu Machi 17, mwaka huu.
Sababu kubwa ya kusimamishwa kwa michezo hiyo nadhani kila mmoja anafahamu, lakini kwa kukumbushia tu ni kwamba, janga la Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 ndiyo imesababisha yote hayo.
Si Tanzania pekee, bali dunia nzima imeathiriwa na Corona kiasi cha kufanya ligi mbalimbali kusimamishwa huku zingine zikifutwa kabisa.
Tayari timu mbalimbali zimeanza mazoezi ya pamoja wiki hii katika kujiandaa na kuendelea kwa ligi ambapo Ligi Kuu Bara imepangwa kuendelea Juni 13, mwaka huu.
Kumbuka Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Kombe la FA ndiyo imeruhusiwa kuendelea.
Tunafahamu kwamba wakati ligi zimasimama Machi 17, mwaka huu, makocha walitoa program maalum kwa wachezaji wao wazifanye kipindi ambacho mechi hakuna kusubiri tamko la kuendelea kwa michuano.
Katika kusubiri kuona ligi zitaendelea lini, ndipo hapo wachezaji wakawa wanafanya mazoezi binafsi bila ya kusimamiwa na makocha wao ikiwa ni sehemu ya kufuata program walizopewa.
Kwa muda wa takribani miezi miwili bila ya kufanya mazoezi ya pamoja, ni wazi wachezaji walikuwa wakijiachia watakavyo ukizingatia kwamba hiki si kipindi cha ‘pre-season’.
Wakati wa mwanzo wa msimu baada ya ule wa awali kumalizika, kunakuwa na mapumziko pale, sasa wachezaji wakienda pre-season, wanaanza wote upya. Hii ni tofauti na sasa.
Inafahamika wazi kwamba kufanya mazoezi binafsi inahitaji moyo sana ni wachache wanaofanya kwa kufuata maelekezo bila ya kusimamiwa. Wengi wao wanaibia.
Kuna wachezaji baadhi kipindi hiki wakiwa nje walionekana bize sana katika kufanya mazoezi maeneo tofauti ili kuhakikisha wanakuwa bora.
Lakini wengine muda huo walitumia kwa mambo yao mengine binafsi bila kukumbuka kazi yao, ila sasa ndiyo wakati wao muafaka kwenda kuonekana kuwa walifanya mazoezi kweli ama ilikuwa ujanjaujanja tu!
Tunaamini yale maneno ya makocha tofauti akiwemo wa Simba kuwa hiki ni kipindi pekee ambacho mchezaji bora ataweza kuonekana uwanjani kwani hawana muda wa kupoteza zaidi ya kuanza ligi.
Ligi itakapoanza ndipo makocha watakuwa makini na kuangalia kuelekea msimu ujao atatakiwa kwenda na nani au kubaki na yupi ndani ya kikosi chake na itategemea na ubora wa wachezaji ambao wataonyesha ndani ya uwanja.
Wachezaji kile ambacho mlichokuwa mnakifanya kwa miezi miwili ambayo mlikuwa nje muda wake muafaka wa kuonekana umefika na hakuna cha kuficha, soka ni mchezo wa wazi, hivyo kipimo cha ubora wenu kitaonekana bila ubishi.
Ni wazi kipute kikianza tutafahamu nani alikuwa anafuata program za kocha kutokana na ufiti wake.
Licha ya kwamba hivi sasa mmeanza mazoezi ya pamoja, lakini kwa muda mchache uliopo hadi kufikia Juni 13, mwaka huu hautatosha kuwafanya mfiche madudu yenu.
0 COMMENTS:
Post a Comment