June 15, 2020



BIASHARA United ni miongoni mwa klabu ambazo zinafanya vizuri kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Bara licha ya kusumbuliwa na tatizo la ukata ambalo limekuwa ni wimbo wa taifa kwao.
Ikiwa na maskani yake mkoani Mara imejijengea ufalme wake ndani ya ligi kutokana na kucheza soka la pasi nyingi huku wakipeta kwenye mechi zao wakiwa na mashaiki wao ambao wamekuwa wakiwapa sapoti mwanzo mwisho.
Ilipanda daraja msimu wa 2018/19 ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Omary Madenge ambaye ni Kocha Msaidizi kwa sasa.Mechi yake iliyoipandisha ilikuwa dhidi ya Transit Camp ambapo ilishinda mabao 3-2 mchezo ulipigwa Uwanja wa Karume, Musoma.
Makocha waliopita Biashara United
Amri Said yupo zake Mbeya City, Hitimana Thiery yupo zake Namungo kwa sasa ipo mikononi mwa Francis Baraza.
Seleman Mataso, Mwenyekiti wa Biashara United anasema kuwa awali ilikuwa timu ya Polisi Mara iliposhindwa kuiendesha timu hiyo ndipo wakaichukua wakati huo walikuwa wakiendesha timu ya Veterani iliyokuwa inataka kuanza kushiriki Ligi Daraja la nne.
Kwa kuwa Polisi Mara ilikuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza waliibadilisha jina na kuipa jina la Biashara United na msimu wake wa kwanza ilipanda jumlajumla na kuaza kushiriki Ligi Kuu Bara.
Mafanikio
Kuwa ndani ya ligi ikiwa ni msimu wake wa pili bila kushuka tangu ilipopanda msimu wa 2018/19.
Kuwa mikononi mwa wananchi ambao wanaiunga mkono timu yao baada ya kukosa timu inayoshiriki ligi ndani ya Mara kwa muda mrefu.
Kuibua vipaji vya vijana wazawa ambao ni hazina kwa taifa hapo baadaye.
Malengo
Kuendelea kupanua wigo mpana kwa wadau na mashabiki ili kuogeza nguvu katika mapato na uimara wa timu.
Kujenga uwanja binafsi utakaowasidia kuwa chanzo cha kipato kwa sasa wanatumia Uwanja wa Karume.
Kujenga hostel ya kisasa ili kupunguza gharama za kambi ambapo kwa sasa timu inakaa kwenye hoteli wakati wa maandalizi.
Kumaliza msimu huu wakiwa ndani ya tano bora.
Kununua gari la kisasa kwa ajili ya safari ya timu kwani kwa sasa usafiri wao huwa ni wa kukodi.
Uwekezaji
Timu imewekeza nguvu kubwa kwa vijana ambao wamekuwa wakiwapandisha kucheza timu ya wakubwa. Lengo kubwa ni kuendelea kubana matumizi ya usajili.
Biashara ya kuuza wachezaji
Mataso amesema kuwa bado hawajaweza kufanya biashara ya maana kwa wachezaji wao kwa sasa ila mipango iliyopo ni kutengeneza timu ambayo itakuwa inatoa wachezaji wengi kwa gharama kubwa ambao wataongeza kuvimba kwa akaunti zao.
 Dau lao la usajili
Kwa mujibu wa Mataso amesema kuwa wakijitahidi sana kuvunja benki wanatoa milioni sita hapo ndipo hesabu zao zinaishia kwa kuwa hawana bajeti kubwa.
“Masuala ya kusajili kwa dau kubwa kwa sasa hilo waachie Simba, Yanga na Azam sisi hatuna gharama kubwa kwa kuwa bajeti haituruhusu.
Mafanikio yao yamejificha hapa
Umoja ndani ya timu, ushirikiano wachezaji na benchi la ufundi.
Mechi inayowapasua kichwa
Mechi dhidi ya Ndanda ambayo ni kiporo kwa sasa inawapasua kichwa sababu tayari waliingia gharama mwanzo kabla ya Serikali kusitisha masuala ya ligi kutokana na janga la Virusi vya Corona.
Mataso anasema:”Mechi yetu dhidi ya Ndanda hapa ni pasua kichwa kwani  gharama zinazohitajika ni  milioni 10 na tayari awali tulikamilisha kwa kufika Mtwara, kabla ya kucheza Corona ikaibuka. Hivyo wadau watambue tunahitaji sapoti katika hili. Hizi nyingine zilizobaki ikiwa ni dhidi ya   Singida United hapa sio mbali gharama zake ni ndogo.
Ilipo kwa sasa
Ipo nafasi ya 10 ikiwa imecheza mechi 29, kibindoni ina pointi zake 40.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic