June 16, 2020



JUNI 13 masuala ya ligi tumeshuhudia yakiendelea pale ambapo yalikuwa yameishia baada ya kusimama kwa muda wa zaidi ya miezi miwili kwenye ardhi ya Tanzania.

Machi 17 nikukumbushe kwamba Serikali iliamua kusimamisha masuala ya michezo na sababu ilikuwa ni kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona ambayo viliitikisa dunia na Tanzania pia.
Ganzi ya kutoshuhudia masuala ya michezo haikuwa Bongo tu hata nje pia ambako huko maendeleo ya teknolojia yamekuwa makubwa pia hakukuwa na shughuli za michezo ambazo zilikuwa zikiendelea.
 Mapambano yalikuwa makubwa ambapo kila mmoja alikuwa akijitahidi kutumia mbinu zake katika kupambana na adui Corona ili kumshinda na kufanya maisha yaendelee kama kawaida.
Haikuwa kazi rahisi kuweza kuyafikia mafanikio kwa namna yoyote kutokana na ugumu ambao ulikuwa upo kuanzia kwa Serikali  na wananchi wenyewe ambao walikuwa kwenye taharuki kubwa kutokana na janga hili.
Hivyo moja ya mbinu ya kivita ambayo ilikuwa ni ya kupambana na Corona ilikuwa ni kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima ili kupunguza maambukizi zaidi ya Corona kwani hali haikuwa salama.
 Serikali yenyewe iliamua kuangalia na kufanya tathimini ni kwa namna gani mambo yanaweza kwenda sawa katika hili kwa kupambania afya za watu wake ambapo iliamua kujitoa kwa nguvu.
Kwa sasa imetangaza kuwa mambo yamekuwa shwari ikiwa inamaanisha kwamba maambukizi yamepungua kwa kiasi kikubwa kwenye ardhi ya Tanzania hili ni jambo jema.
 Kutokana na kupungua kwa maambukizi, Serikali imeamua kuruhusu masuala ya michezo kuendelea pale ambapo ilikuwa imeishia hivyo burudani ambayo tuliikosa kwa muda mrefu inarejea.
Muhimu kutambua kwamba dunia bado inapambana kuendelea kurejea kwenye usawa wake huku ikipambana na janga la Corona ambalo sio jepesi kama ambavyo wengi wanafikiria.
Tayari utaratibu umeanza kurejea kama ilivyokuwa awali ambapo kazi kubwa ilikuwa ni kuchukua tahadhari dhidi ya Corona na kuamua kuendelea masuala ya michezo ambayo yalisimama kwa muda zaidi ya miezi miwili.
Ninaona kwamba wengi wanafurahi kurejea kwa masuala ya michezo hata mimi nimefurahi pia lakini ninaona kuna ile hali ya kupuuzia ambayo imeanza kuonekana kwa sasa kwenye ulimwengu wa michezo pamoja na maisha ya kawaida.
Kauli ya kurejea kwa masuala ya michezo haina maana kwamba Corona imekwisha bado janga hili lipo na ni lazima tuendelee kuchukua tahadhari ili kuwa salama muda wote.
Jambo la msingi ni kila mmoja kuendelea kuchukua tahadhari na kufanya mambo ya msingi kwa ajili ya afya yake mwenyewe pamoja na jamii nzima inayomzunguka.
Sitachoka kuwakumbusha ndugu zangu kwa kuwa ni muhimu hili likawa kwenye akili zetu kwamba kinga ni bora kuliko tiba kwa kutambua hili itatufanya tuwe salama muda wote.
Kwa kuwa ligi inarudi basi muongozo ambao umetolewa ni muhimu kufuatiliwa bila kukosea hata kidogo masuala ya kurejea uwanjani na adhabu hata haipendezi hata kidogo kwa kweli.
Kinachotakiwa ni kuona namna gani burudani itaendelea kutolewa huku ule ushauri na maelekezo ya kitaalamu yakifanyiwa kazi na kila mmoja ambaye ni mdau wa michezo.
 Hapa ngoja tukumbushane kwanza kidogo mambo ya msingi ambayo yapo kwenye muongozo ambao umetolewa na Serikali kuhusu kurejea kwa ligi kwamba ni pamoja na kila mdau ambaye atapenda kwenda uwanjani kushangilia timu yake anayopenda kuvaa barakoa.
Hii barakoa ni muhimu kuzingatia kwa kila shabiki unaweza ukapuuzia na ukashangaa unaishia getini kisha ukabaki unalaumu kumbe utaratibu ulipewa mapema na kila kitu ulikuwa unajua.
Ili usikutwe na janga la namna hii ndugu yangu wewe anza kununua barakoa yako sasa kwani muda bado upo na njia nyepesi unaweza ukashona wewe mwenyewe bila kuogopa na ukawa miongoni mwa wale wenye barakoa hapa mjini.
Mamlaka inayosimamia michezo Tanzania, Shirikisho la Soka (TFF) ni wakati wa kutazama namna bora katika kusimamia msimu wa 2019/20 pamoja na muongozo ambao umetolewa kwa wadau wote wa michezo ili uzingatiwe kwa umakini.
Mechi zilizobaki kwa sasa ni chache na kila mmoja atakuwa anahitaji kushinda hivyo muhimu kutazama mbinu ambazo zitatumika kutafuta ushindi pamoja na afya za watazamaji kwa wakati mmoja.
Pia jambo lingine ambalo lipo kwenye muongozo ni kuhusu umbali wa mita moja, hapa ni katika nyakati zote zile za kuingia ndani ya uwanja na kutoka nje ya uwanja.
Muhimu kila shabiki na mdau wa michezo akatambua kwamba anatakiwa kukaa umbali wa mita moja na mwenzake wasiwe karibukaribu kwani wakati huu usalama bado haujawa mkubwa kwa kiasi hicho..
Tukumbuke kwamba Serikali yenyewe imesema kwamba bado Corona ipo na muhimu kuchukua tahadhari hatupaswi kupuuzia eti kwa kuwa tunaingia uwanjani kushangilia na kuona mpira ukiendelea.
 Pia jambo lingine ambalo ningependa kuwakumbusha ni kuhusu suala la kunawa kwa maji tiririka kwani hili lipo siku zote na limekuwa likifuatwa na wengi baada ya janga hili naona kidogo mambo yameanza kubadilika.
Napenda kuwaomba pia bado tusijisahau kiasi kikubwa na kuendelea na mambo yale ambayo tulikuwa tukiyafanya zamani hapa muda wake umeisha ni wakati wa kutazama namna gani tutafuata kanuni na muongozo ambao umewekwa.
Hii yote ni tahadhari kwani Corona bado ipo pia wasijisahau kwamba wanatakiwa kunawa na maji tiririka, kukaa umbali wa mita moja hili nalo ni la msingi kuzingatia kuelekea kurejea kwa ligi.
Mwisho japo sio kwa umuhimu sana ni kwamba kila mmoja ajitahidi awe na sanitizer yake mwenyewe hili pia ni kwa usalama wa afya yako kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Tusijisahaulishe kwa kuwa tatizo linaelezwa kuwa limepungua basi tukaamua kabisa na kusahau kufanya ibada na dua hili sio sawa ni lazima tuendelee kumuomba Mungu wetu usiku na mchana bila kuchoka.
Ninaamini iwapo kila mmoja atafuata ile njia ambayo inatolewa na Serikali kisha akaendelea kufanya dua usiku na mchana wote kesho tutakutana tukiwa salama na tukipongezana kwamba tumeweza kupenya kwenye nyakati ngumu za Corona.
Ugonjwa huu upo  kweli hilo tusijisahau kwa kuendelea kuishi maisha yale ambayo tuliyazoea zamani ni muda wa kubadilika na kuongeza umakini zaidi.
Timu nyingi kwa sasa zinaendelea na maandalizi yake kwa ajili ya kumalizia mechi zao za lala salama hili ni jambo la msingi kwani lazima kuwe na maandalizi mazuri ili kufikia malengo.
Kwa wakati huu kuna timu ambazo zisipoangalia vema na kuchanga karata zao basi zitakuwa sehemu ambayo hazikutegemea wakati ule ligi itakapokwisha.
Jambo la msingi ni mipango makini ambayo itawasaidia wachezaji kuwa kwenye ubora wao pamoja na utayari wa kuendeleza vita ya ndani ya uwanja ya kutafuta matokeo.
Wachezaji wakati wenu wa kurejea uwanjani tayari umeshafika na nina amini kwamba muda ambao mnafanya mazoezi na timu ni lazima mtarejea kwenye ubora wenu.
Kila mchezaji asijisahau kwa kufikiri kwa kuwa alikuwa kwenye mapumziko akadhani na majukumu yatapumzika hapana lazima mapambano yaendelee.
Tunaamini kwamba kwa sasa kazi kubwa itakuwa ndani ya uwanja kupambana na kutafuta matokeo kwa ajili ya timu zao ndani ya uwanja bila kuchoka.
Dakika tisini kwa sasa ndio atakuwa mwamuzi wa kile ambacho mlielekezwa kufanya mkiwa kwenye mapumziko na inapaswa iwe katika umakini mkubwa kutimiza majukumu yenu.
Ushindani lazima utakuwa mkubwa kwani timu ambazo zinashuka daraja ni nyingi na zile ambazo zinahitaji kubaki ndani ya ligi pia ni nyingi hivyo lazima kazi iendelee kutafuta matokeo.
Ninaona kwamba kila mchezaji anakwenda kuvuna kile ambacho alikipanda huku walimu pia wakienda kumaliza ile ngwe ambayo walikuwa wameaianza awali kabisa.
Mambo yatakuwa hadharani kwa kila mchezaji kuonyesha makeke yake ndani ya uwanja na kuwapa mashabiki kile ambacho alikuwa akikifanya bila mashaka yoyote.
Burudani inarejea na kila mmoja ataona namna gani ndani ya siku ambazo wachezaji walikuwa wakiishi kwa namna yoyote ile kutokana na vita ya Corona ambayo wengi imekuwa ni kivuli cha kujificha wasifanye mazoezi.
Kujificha kwenye Corona haina maana kwamba utakuwa salama hapana ni lazima upambane ndani ya uwanja ili uwe bora zaidi ya jana jambo ambalo litakufanya usiwe mzembe.
Uongozi wa timu pia ni wakati wa kukamilisha ile mipango ambayo ilikuwa imepangwa awali kwa kukamilisha mambo yanayowahusu wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Kusiwe na sababu ya kushindwa kufikia mafanikio kisa jambo fulani halikufanywa hapana haitaleta maana njema kwa wakati huu ambao tupo ni muhimu kila kitu kikawekwa kwenye mpangilio mzuri.
Juhudi zinahitajika katika kuwatimizia majukumu wachezaji ili nao pia wawe na juhudi katika kutimiza kile ambacho uongozi unahitaji kwa namna yoyote.
Jambo la msingi ni kuzingatia kwambaCorona ipo na tahadhari inatakiwa kuendelea kuchukuliwa bila kuchoka.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic