KWA kasi ya msimu wa 2020/21 ilivyoanza nina amini kwamba tutashuhudia mambo mengi sana hasa ndani ya uwanja.
Inapendeza
kuona namna ambavyo timu zinafanya vizuri ndani ya uwanja katika kutafuta matokeo.
Kwa namna ambavyo Ligi Kuu Tanzania Bara imeanza inavutia.
Itakuwa
vizuri ushindani huu ukiendelea mpaka mwisho wa msimu. Sio kwa kuwa ni mwanzo
basi timu zikakamia mwanzo kisha mwisho zikajisahau haitapendeza.
Muda uliopo
sasa ni kila timu kupambana na kuendelea kujiandaa kwa mechi ambazo ipo nazo
mbele kwani safari ndo kwanza inaanza.
Ninaona
kwamba mashabiki nao pia wapo mbele kwa kujitokeza ndani ya uwanja. Hakika
mnastahili pongezi hapahapo mliposhika endeleeni wala msirudi nyuma.
Septemba 6 na
7 baada ya mechi 9 kuchezwa kukamilisha mzunguko wa kwanza tumeshuhudia
mashabiki wakijitokeza kushangilia timu zao wanazozipenda.
Dakika 90
ni muda sahihi uwanjani na unatatosha kuwapa burudani mashabiki na kushuhudia
uwezo wa wachezaji wao ambao wapo baadhi ni wapya baada ya dirisha la usajili
kupita.
Ukiachana
na mashabiki kujitokeza kuwaona wachezaji wao pia wanahitaji ile ladha ya soka
iwe endelevu yaani tamu mwanzo mwisho bila kuharibiwa na maamuzi ya waamuzi.
Ili waamuzi
wasiweze kuboronga katika kutoa ile ladha kazi yao iwe moja tu ndani ya uwanja,
kufuata sheria 17 za mpira.
Kwa kufanya
hivyo mashabiki wetu ninawatambua linapokuja suala la haki wanaelewa sana na
wanapenda kuona timu zao zinashinda kwa uhalali kabisa.
Nakumbuka
kuna shabiki aliwahi kuniambia kwamba ni kheri timu yake ikafungwa kwa uwezo
ama ikashinda kwa uwezo ila sio kwa mabao ya kuonyesha kwamba wamebebwa huwa
inamnyima usingizi.
Kweli
maamuzi ya waamuzi wakati mwingine huwa yanakuwa tofauti ndio maana tunaona
msimu uliopita wapo ambao waliadhibiwa kwa kufungiwa mechi kadhaa na wengine
walipewa onyo.
Kwa msimu
huu mpya, yale yaliyopita kwa waamuzi kufungiwa ama kupewa adhabu hatuhitaji
kuskia tunataka kuona mwamuzi baada ya mchezo naye awe anapewa pongezi.
Tunahitaji
kuona kwamba kila mchezaji anatoka ndani ya uwanja akiamini kwamba amepoteza
kutokana na makosa ya timu ambayo yamewagharimu na sio kumbebesha lawama
mwamuzi.
Kwenye
mechi za ufunguzi kelele za hapa na pale huwa hazikosekani lakini zifungue
mwanga kwa waamuzi waweze kuangalia pale ambapo wanakosea ili wajifunze zaidi.
Makosa yapo
kwa kila mmoja kuanzia wachezaji, waamuzi, mashabiki mpaka wale waokota mipira
nao wana makosa yao lakini haitapaswa yawe endelevu lazima yafanyiwe kazi.
Kwa kufanya
hivyo na kujifunza zaidi kwa waamuzi kufuata sheria 17. Ikiwa hivyo tutakuwa na
ligi bora mfano wake hakuna hata bingwa atakayepatikana atafurahiwa na dunia
nzima kwa kuwa kila kitu kiliendeshwa kwa haki.
Ujumbe wangu
kwa timu ambazo zimepanda daraja kwa msimu wa 2019/20 zikiwa na uhakika wa
kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/21 zina kazi ya kupambana.
Gwambina FC
na Ihefu zimeanza kwa kupoteza bado zina nafasi ya kurekebisha makosa na
kufanya vema kwenye mechi zao zinazofuata.
Dodoma
Jiji hawa wameanza kwa ushindi mbele ya Mwadui FC wanapaswa pongezi hata wale
waliopoteza pia wanapaswa pongezi kwani wameonyesha ushindani wa kweli.
Ishu ya kushuka daraja bado ipo hivyo ni
muhimu kulitambua hilo wakati ligi ikiwa imeanza kusonga mbele taratibu.
Singida
United,Lipuli FC,Ndanda FC,Alliance na Mbao zipo kwenye ulimwengu mwingine wa
Ligi Daraja la Kwanza zikijiandaa kurejea tena huku kwenye ligi.
Jambo la
msingi ni kwa kila timu kuweza kutimiza majukumu yake vizuri ndani ya uwanja.
Maandalizi mazuri katika kila mchezo yatawapa matokeo chanya.
Kila timu
kwa sasa inaweza kupata matokeo chanya hata ikiwa ugenini licha ya kwamba na
zenyewe ni ngeni cha msingi ni kukubali kwamba mmeshapanda na mnahitaji
ushindi.
Imani yangu
ni kwamba baada ya kila timu kucheza mchezo mmoja kuna kitu ambacho kitakwenda
kufanyiwa maboresho.
Katika
maboresho hayo msisahau kwamba wapo ndugu zenu pale Ligi Daraja la Kwanza nao
wanahitaji nafasi hivyo kwa kulitambua hilo nina amini kutawapa nguvu ya
kupambana zaidi.
Maisha ya
Ligi Daraja la Kwanza tayari kwenu muda wake umeisha kwa sasa pambaneni kuweka
rekodi mpya. Iweni kama Namungo namna ilivyoleta ushindani na ilimaliza ndani
ya tano bora.
Polisi
Tanzania pia nao walifanya vizuri kwa kumaliza ndani ya tano bora ikiwa ina
maana kwamba hata nyinyi mnaweza pia. Jifunzeni kwa wale ambao wameweza kufikia
hatua ambazo mnazihitaji.
Wachezaji
ndani ya uwanja ni muhimu kupambana kwa hali na mali kusaka ushindi ili kuwapa
wanachostahili mashabiki wenu.
Kwa kufanya
kwenu vizuri ndani ya uwanja kunawapa nguvu mashabiki kuendelea kujitokeza
ndani ya uwanja kila iitwapo leo na inapendeza kuona kwamba wameanza kujitokeza
kwa wingi.
Sapoti ya
mashabiki ndani ya uwanja ni kubwa na ina umuhimu hivyo ili waendelee
kujitokeza kwa wingi uwanjani ni lazima matokeo yawe mazuri.
Ikishindikana
kwa matokeo ndani ya uwanja basi wachezaji chezeni kwa kuonyesha viwango bora
ndani ya uwanja hili pia ni jambo la kuzingatia.
Furaha ya
mashabiki inabebwa na ushindi pamoja na kushuhudia ule udambwiudambwi ndani ya
uwanja kwa wachezaji kuonyesha uwezo mwanzo mwisho.
Matumaini
yangu kutakuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote ndani ya ligi pamoja na
mashabiki kuendelea kujitokeza kwa wingi.
Mwamuzi atafuataje sheria 17 wakati sheria nyingine hazimhusu mwamuzi kama suala la hali na vipimo vya uwanja?
ReplyDelete