KIKOSI cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Zlatko Krmpotic leo Septemba 18 kimefanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo wake wa kesho dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa majira ya saa 10:00 Uwanja wa Kaitaba.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na matokeo ya Kagera Sugar kuwa ya kusuasua kwa msimu huu, kwa kuwa inataka kurejea kwenye ubora wake, huku Yanga ikiwa inahitaji kurejesha heshima kwa kusaka pointi tatu ikiwa nje ya Dar.
Kagera Sugar ilianza kwa kususasua baada ya kukubali kufungwa bao 1-0 mbele ya JKT Tanzania Uwanja wa Kaitaba kisha mechi yake ya pili ikalazimisha sare ya bila kufungana na Gwambina FC, Uwanja wa Gwambina.
Yanga inaingia kwa kujiamini kwa kuwa imetoka kushinda mbele ya Mbeya City bao 1-0 pia kwenye mchezo wake wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ilishinda kwa mabao 2-0.
Hafidh Saleh, meneja wa Yanga amesema kuwa kikosi kipo kamili kwa ajili ya mchezo wa kesho na wanachohitaji ni pointi tatu muhimu.
"Tupo vizuri kwani tulipofika huku tuliaza kufanya mazoezi na tunaendelea salama, kikubwa tunahitaji pointi tatu muhimu," amesema.
Ni kweli point 3 kwetu muhimu
ReplyDelete