KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amesema kuwa amefurahishwa na kuridhishwa na matokeo ya ushindi kwenye mechi zake mbili alizokaa kwenye benchi akiifundisha timu hiyo.
Kaze mchezo wake wa kwanza alishinda bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, Uwanja wa Uhuru na mchezo wake wa pili alishinda mabao 2-1 dhidi ya KMC Uwanja wa CCM Kirumba.
Kocha huyoamesaini dili la miaka miwili akichukua nafasi ya Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyesitishiwa mkataba wake Oktoba 3.
Kaze amesema kuwa bado anataka kuona timu yake ikiendelea kucheza soka safi la pasi na kasi wakati timu ikiwa na mpira.
“Nimepokea pongezi nyingi kutoka kwa mashabiki wa Yanga wakinipongeza kwa timu kuonyesha mabadiliko kidogo hasa timu ikiwa na mpira ngumu kuupoteza huku tukishambulia goli la wapinzani muda wote.
“Niwaambie mashabiki wa Yanga kuwa, huo ni mwanzo tu bado mengi yanakuja kama unavyofahamu nimekaa na timu muda mchache, hivyo kuna vitu vya kuboresha ili kuhakikisha timu inacheza soka lile ninalolitaka mimi la pasi nyingi na kasi.
“Hivi sasa nazifanyia kazi baadhi ya sehemu zenye upungufu ikiwemo safu ya ushambuliaji ambayo yenyewe inaonekana kushindwa kutumia nafasi nyingi na hiyo ni kutokana na timu kutokuwa na muunganiko mzuri tunapofika goli la mpinzani.
“Kingine ni kuwa timu inakuwa haina haraka kutafuta mpira pale tunapopoteza. hivyo tunajipanga kukabiliana na mchezo mmoja mmoja,” amesema Kaze.
Ikiwa imecheza mechi saba ina pointi 19 ipo nafasi ya pili kinara ni Azam FC mwenye pointi 21 baada ya kucheza mechi nane.
0 COMMENTS:
Post a Comment