KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Said Ntibazonkiza, amesema timu hiyo ilianza kumfuatilia miezi miwili hadi mitatu iliyopita kabla ya kufikia makubaliano ya kusaini mkataba huku akitamba ametua kwa kazi moja tu ya kusaidia timu kutwaa mataji.
Ntibazonkiza alisajiliwa na Yanga Oktoba 12 kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu akiwa mchezaji huru ambapo vijana hao wa Jangwani walimnasa baada ya kumalizika mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Tanzania dhidi ya Burundi uliomalizika kwa Burundi kupata ushindi wa bao 1-0.
Bao la ushindi kwa Burundi ambalo liliacha ganzi kwa Watanzania Uwanja wa Mkapa, Oktoba 11 lilifungwa na yeye mwenyewe Ntibazonkiza.
Kwa mujibu wa Ntibazonkiza amekiri ujio wake katika timu hiyo, kocha mpya Cedric Kaze amehusika kwa asilimia mia moja kutokana na kuwahi kumfundisha kwenye timu ya Taifa ya Burundi, mwaka 2011.
“Mimi nimekuja Yanga sio kwa bahati mbaya, wapo wanaofikiria nimesajiliwa baada ya mchezo dhidi ya Tanzania.
"Tulikuwa na mazungumzo na Yanga miezi miwili au mitatu nyuma.Lakini nilishindwa kujiunga nao kutokana na changamoto kadhaa zilizokuwepo wakati huo. Sasa nilipokuja tena hapa ikawa rahisi kumalizana nao kwani hata yale yaliyotukwamisha mwanzo hayapo," amesema.
0 COMMENTS:
Post a Comment