October 27, 2020



Na Saleh Ally

YANGA imecheza na KMC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Oktoba 25 wakati timu hizi zote zinatokea jijini Dar es Salaam.

 

KMC ndio walikuwa wenyeji wa mchezo huo baada ya kuamua kuuhamishia huko kwa mujibu wa kanuni za Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

 

Kanuni hiyo ya TPLB, inatoa nafasi kwa timu kuhamisha michezo angalau miwili kwenda katika moja ya viwanja ambavyo havichezewi Ligi Kuu Bara kwa msimu husika.

 

TPLB waliamua kufanya hivyo kuzisaidia klabu kadhaa ambazo zilikuwa zikilalamika kwamba kucheza Dar es Salaam pekee kumekuwa hakuna mapato.

 

Klabu kadhaa zililalamika zikiwemo hata Yanga na Simba ambazo awali zilikuwa zikilalamika kuhusiana na suala la ukosefu wa mapato hasa baada ya kupitishwa ile kanuni kuwa kila timu itachukua mapato yote ya nyumbani.

 

Awali, ilikuwa timu zinagawana kwenye kila mchezo. Lakini mabadiliko yakapita na ikapitishwa kutumika kuwa mwenyeji achukue mapato yote na malalamiko yakaanzia hapo.

 

Baada ya kuona hivyo, TPLB wakaona kama wanaweza kulainisha mambo kwa kwa kuwapa nafasi waliolalamika kuangalia namna ya kuongeza hayo mapato na hasa kupeleka mechi kwenye viwanja ambavyo wanaona kuna uhitaji wa watu kuwaona.

 

KMC wao wameona wakiwapeleka Yanga Mwanza, watu watakuwa wanahitaji kuwaona ukizingatia ni mara ya kwanza kwa msimu wa 2020/21, hivyo wanajua kabisa wataingiza fedha za kutosha.

 

Kila mmoja anajaribu kuangalia njia za kumuingizia kipato, KMC unaona wamechangamka. Na kanuni hii, unaona kabisa kupitia wao TPLB, lengo linakuwa ni kuzisaidia timu kuingiza kipato cha kutosha zaidi.

 

Pamoja na nia nzuri ya TPLB kwa kushirikiana na wao klabu kama wadau namba moja, kuna sababu ya nguvu kuongezwa katika kanuni hii ili kuipa nguvu ya kulinda kile ambacho kimekusudiwa.

 

Kwamba kama klabu inataka klabu nyingine kwenda kucheza kwenye uwanja ambao haukuwa umepangwa kwa kuitumia kanuni hiyo, basi kuwe na uhakika lengo ni hilo na si urekebishaji wa matokeo.

 

Nasema hivi ili hili liangaliwe pale inapotokea kuna timu zinakaribia kuteremka daraja au kuwania ubingwa na moja ikaona kuichosha nyingine kwa kuipeleka mbali kutokana na uwezo mdogo au kwa kuwa baada ya mechi ya Mwanza basi itakwenda kucheza Mbeya siku tatu zinazofuata, haitakuwa sahihi.

 

Hofu yangu kanuni hii ambayo kwingine haipo, isitumike kama sumu ya kuwaumiza wengine. Lengo ni kuzisaidia klabu kuongeza kipato na kuweza kujiendesha vizuri na si kuitumia kumfanya mmoja awe dhaifu au mbinu ya ushindi.

 

Inawezekana pia timu moja ikashirikiana na nyingine kuipa moja ya timu safari, ikirejea itaikuta nyingine ikiwa katika nafasi nzuri na imepumzika ili iwe rahisi kuishinda.

 

Haya yote ninaamini hayajafanyika lakini watu wa mpira kila kukicha wanajaribu jambo jipya na mara kadhaa tumeona kitu kimeundwa kwa ajili ya kunufaisha mpira wenyewe lakini kinatumika vibaya.

 

Ninaona ni jambo la kujifunza na kwa kuwa TPLB walikianzisha kwa nia nzuri na wakakubaliana na wadau wao ambao ndio klabu, bado tunapaswa kusema ni jambo zuri lakini matumizi yanaweza kuwa mabaya ndiyo maana nayawekea msisitizo kuwa kuwe na namna ndani ya kanuni hiyo kuhakikisha nia au lengo hilo la matumizi sahihi linafanyika.

 

Unaona kama Yanga wamepata bahati, wakati KMC wakiwahamishia Mwanza, baada ya mechi ya CCM Kirumba, mechi yao inayofuatia ni Mara dhidi ya Biashara na baada ya hapo watarejea Mwanza tena, itakuwa ni nafuu kwao na lengo unaliona ni mapato na huku ndiko kutimiza lengo.

2 COMMENTS:

  1. TFF hawana nia nzuri kwa vilabu au wapenzi wa soka utapangaje mechi jumatatu au alhamisi?si unawakomoa vilabu

    ReplyDelete
  2. Ulicho kisema kizuri tff nao waliangalie kwa upana hili

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic