BAADA ya msimu uliopita ngoma kuwa ngumu ambapo kwa dakika zote 180 hakukuwa na bao lolote lililofungwa kati ya Simba na Prisons, leo Alhamisi miamba hiyo itakutana katika Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa kumaliza ubishi.
Mchezo wa kwanza msimu uliopita ulipigwa Novemba 7, 2019 jijini Dar na kumalizika kwa suluhu, huku ule wa pili uliopigwa Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, ukiisha kwa suluhu pia.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema: “Mpaka leo (jana) wachezaji wote waliosafi ri na kikosi kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Prisons wako salama.
“Malengo yetu ni kuhakikisha tunaendeleza matokeo ya ushindi, hivyo tutaingia kwa tahadhari kubwa kwenye mchezo huu hasa kwa sababu tunajua ubora wa wapinzani wetu.
”Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Prisons, Salum Mayanga, alisema: “Kikosi kipo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Simba, tunajua ugumu uliopo kucheza na Simba, lakini hilo halitupi wasiwasi, tumejipanga kuhakikisha pointi zote tatu wanaziacha Sumbawanga.
“Mashabiki wetu watarajie mambo mazuri kwani wachezaji wamejipanga kupambana kwa ajili ya kuchukua pointi tatu.”
Rekodi zinaonesha kuwa, timu hizo kuanzia msimu wa 2012/13, zimekutana mara 16 kwenye Ligi Kuu Bara, Simba imeshinda mechi kumi, Prisons imeshinda mbili na sare nne.
0 COMMENTS:
Post a Comment