JURGEN Klopp, Kocha Mkuu wa Liverpool amesema kuwa kwa sasa nyota wake wawili ambao ni Sadio Mane na Thiago Alcantara wapo fiti baada ya afya zao kutengamaa baada ya kukutwa na Virusi vya Corona.
Nyota hao wote wawili wanatarajiwa kuanza kufanya kazi rasmi leo Oktoba 17 wakati timu yao ya Liverpool itakapokuwa ugenini ikicheza mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Everton.
Mchezo huo ambao ni dabi ya Merseyside itachezwa uwanja wa Goodison Park majira ya saa 8:30 mchana inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili ambapo kasi ya Everton imekuwa ni kali baada ya kushinda mechi zake zote nne nne ikiwa nafasi ya kwanza na pointi 12.
Everton ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Carlo Ancelotti ipo vizuri ndani ya uwanja na hasa ikiwa nyumbani ina pewa nafasi ya kushinda mchezo wa leo baada ya Liverpool kutoka kubamizwa mabao 7-2 na Aston Villa.
Klopp amethibitisha kwamba Mane na Thiago wamerejea kwenye kikosi na hawaonyeshi dalili zozote za Corona kwa sasa baada ya kuwa chini ya uangalizi.
"Wamekuwa pamoja nasi kwa muda wa zaidi ya siku sita zilizopita kwenye mafunzo na kila siku tumekuwa tukiwatazama maendeleo yao na inaleta matumaini, wanaonekana wapo vizuri," amesema.
0 COMMENTS:
Post a Comment