November 5, 2020

 


ILIKUWA mwezi, wiki, hatimaye sasa ni siku moja imebaki kabla ya dunia kushuhudia ile dabi ya Kariakoo. Watani wa jadi Yanga na Simba wanatarajiwa kukutana Novemba 7.

Kila mdau na shabiki kwa sasa ni mshindi kwa kuwa anaona namna wachezaji wake wanavyopambana ndani ya uwanja kusaka matokeo.

Kwenye mechi zao ambazo zimepita kila kitu kipo wazi na ninaamini kwamba maandalizi ya timu zote mbili yapo vizuri suala la kupeperuka tena dabi mwezi huu hilo inaonekana hakuna tena.


Awali ilitarajiwa kuchezwa Oktoba 18 Uwanja wa Mkapa ila mambo yalibadilishwa na Bodi ya Ligi Tanzania,(TPLB) kwa kile ilichoeleza kuwa hofu ya usafiri kwa wachezaji ambao waliitwa kwenye timu zao za taifa.


Kikubwa ambacho kinatakiwa kwa mashabiki ni kuwa watulivu na kuwaacha walimu wafanye yao ila wao jukumu lao ni moja tu kujitokeza uwanjani kuzipa sapoti timu, basi hakuna kingine.


Wachezaji wakati wenu huu sasa kushusha presha kwa mashabiki. Ugonjwa wa mashabiki ni kuona mpira mzuri achana na pira gwaride ama pira kashata weka pembeni mpira mzuri unahitajika.


Masuala ya ugomvi ndani ya uwanja kwa kuwa ni dabi kwa wachezaji tupa kule chezeni mpira ndicho ambacho kinawafurahisha mashabiki kisha mkicheza kwa ustaarabu matokeo yatakayopatikana yatawafanya mashabiki kuwa na furaha.


Utamaduni wa Tanzania namba moja ni upendo hivyo ninaamini kwamba hakutakuwa na ugomvi kuanzia kwa mashabiki na wachezaji pia. Utulivu unahitajika wakati wa kuzipa sapoti timu hizi mbili ambazo ni timu pendwa.


Pia kwa mashabiki kwa wakati huu hamtakiwi kubeba matokeo mfukoni na kuamini kwamba yatatokea, hilo jambo nakushauri ndugu yangu, rafiki yangu futa kabisa akilini  mwako.


Kwa mwendo wa ligi hii, mwenyeji anapigwa na mgeni pia anapigwa hivyo sio mwenyeji mwenye uhakika wa ushindi wala mgeni mwenye uhakika wa ushindi, dakika 90 zitaamua nani ni nani.


Waamuzi pia kwa sasa mna wimbo wenu mpya ambao mpo nao kwa wakati huu kazi ni kwenu sasa kuuimba kwa uzuri wimbo wenu wa sheria 17.



Hakuna mtihani mgumu kwa wakati huu kuchezesha dabi ambayo inafuatiliwa na dunia nzima. Umakini unahitajika na sheria 17 muhimu kufuatwa.


Ikitokea mwamuzi akaboronga ni rahisi kuzomewa ama kusababisha vurugu jambo ambalo hakuna Mtanzania anayependa kuona tunafikia hatua hiyo.


Masuala ya kuboronga makusudi kwa kuwa kuna adhabu eti za kufungiwa ama kuonywa hilo lisipewe kipaumbele muhimu kufuata sheria 17 za mpira.


Ninaona wachezaji wapo ambao wamepania kufanya maajabu, kikubwa ni maandalizi kwa timu zote kuanzia benchi la ufundi, wachezaji wenyewe wanapaswa waache matokeo yao nyumbani na kuamini kwamba matokeo yatapatikana ndani ya dakika 90.

Kila timu na ifanye kazi katika kufanya maandalizi mazuri na kuweka saikolojia za wachezaji katika usawa ili kuondoa zile presha.

Matukio mengi yamekuwa yakitokea na kufanya wengi wasiamini matokeo ambayo yatatokea, mpira una mambo mengi, tukutane Novemba 7.


Mashabiki ni muhimu kuwa watulivu na kuzipa sapoti timu zenu ndani ya uwanja kuona burudani itakavyokuwa.


Wachezaji mna kazi ya kutoa burudani kwa kucheza vizuri mpira uwanjani zile butuabutua hazipaswi kupewa nafasi bali utulivu kwa kila timu kutawafanya mzidi kuwa imara.


Jambo jingine ni kwamba mchezo huu ni fursa kwenu kujiweka kwenye orodha ya wachezaji ambao wataingia sokoni kwa wakati ujao.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic