PONGEZI kubwa kwa maofisa habari wa timu
zote zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Wanawake
pamoja na Ligi Daraja la Pili.
Kazi yenu nyepesi na nzuri kwa sababu
mmeichagua hivyo nikisema ni ngumu nitakuwa ninawaongopea ila ni nzuri na
inaonekana kwa jamii kutokana na kile ambacho mnakifanya.
Mazuri yapo kwa mwaka 2020 ambapo kila
mmoja amekuwa na njia yake ya kipekee katika kuwakilisha taarifa kwa mashabiki
pamoja na wale ambao wanawafuatilia.
Wakati mwingine pia kumekuwa na uzinguaji
ndani ya mwaka 2020 ila hayo inapaswa yaachwe 2020 na kufungua ukurasa mpya
2021.
Haji Manara, Ofisa Habari wa Simba
anastahili pongezi kwa jitihada zake za kuitangaza Simba na jitahada zake
zinaonekana.
Mkongwe Thobias Kifaru wa Mtibwa Sugar ni
moja ya maofisa habari ambao wanajali muda na kutoa kile ambacho kinahitajika
kwa mashabiki wake pamoja na wale ambao wanaifuatilia timu yake.
Nakumbuka zama zile nikiwa nasoma masuala
ya uandishi wa habari nikiwa na ndugu yangu Gwamaka Mwakanyamale ilikuwa
tukiskia Kifaru anaongea lazima wote tukae kimya kisha tuanze kumsikiliza.
Alishinda mabao 4-0 dhidi ya Majimaji
kumbukumbu zangu zinaniambia akasema:”Tunasikitika kuwaambia mashabiki
wetu kwamba tumeshinda kwa ushindi mwembamba wa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji,” ,
Hakika kazi yako inapendeza, ukija kwa
Masau Bwire yeye ni mzee wa kupapasa. Muda wote amekuwa akitoa ushirikiano kwa
vyombo vya habari bila ubaguzi na hata akifungwa haishiwi maneno na tambo zake.
Ukimuweka kando huyo pia Thabit Zakaria
ndani ya Azam FC pia amekuwa imara katika kukuza kitengo chake cha taarifa na
hana tatizo na mwandishi pia kupitia ukurasa wao wa Instagram imekuwa ni rahisi
kukuta kazi za vyombo mbalimbali vya habari.
Ukigusa Yanga hapa hawa wanaye Hassan Bumbuli ambaye amekuwa akiendelea kuendesha gurudumu ndani ya kikosi hicho.Anachonifurahisha ni kwamba wakati mwingine ukihitaji kumuhoji kuhusu masuala ya Yanga atakuambia hilo tutaweka kwenye mitandao ya kijamii.Kwangu mimi naona sio sawa kwa sababu anapaswa kutoa ushirikiano kwa kile ambacho anaulizwa.
Kwa JKT Tanzania wanaye Jamila Mutabazi pia
kwa KMC yupo Christina Mwagala hawa ni maofisa ambao ni wapambanaji nao wanastahili pongezi.
Ligi ya Wanawake kwa JKT Queens uwepo wa
Cpl Elizabeth Buliba, Baobab Queens yupo Timotheo Francis wote ni wapambanaji.
Wengi tunatambua mchango wenu na mnastahili
pongezi kwa kuwa mnafanya kazi kubwa hivyo kwa yale ambayo yalifanyika 2020 kwa
makosa ni wakati wa kuyaboresha ili kuwa bora kwa mwaka 2021.
Imani yangu ni kwamba kila mmoja mbali na
hawa maofisa habari ambao wengine sijawaorodhesha hata wewe msomaji pia umekuwa
nasi bega kwa bega ndani ya mwaka 2020 nawe pia unastahili pongezi.
Tuzidi kushirikiana pia kwa mwaka mpya wa
2021 kwa kuwa wahenga walituachia ujumbe kwamba umoja ni nguvu na utengano ni
udhaifu.
0 COMMENTS:
Post a Comment