NYOTA wote wa Yanga akiwemo staa mpya wa kikosi hicho, Said Ntibazonkiza ‘Saido’, wamepewa masharti magumu katika mzunguko huu wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Masharti hayo ni kuhakikisha wanaendeleza rekodi yao ya kutopoteza mechi katika ligi, huku wakiambiwa wasahau mechi zilizopita na badala yake kuangalia kilicho mbele yao ili kufikia malengo.
Yanga inaongoza Ligi Kuu Bara hivi sasa ikiwa na pointi 44, msimu huu imepania kufanya kweli kuhakikisha inatwaa ubingwa huo ilioukosa kwa misimu mitatu na kutua kwa watani zao wa jadi, Simba.
Akizungumza na Spoti Xtra, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, amesema kuwa, uongozi na benchi la ufundi limekutana na wachezaji kwa ajili ya kuwataka wasahau matokeo ya mzunguko wa kwanza ili kuanza na kasi mpya katika mzunguko wa pili.
“Mikakati yetu ni kuanza mzunguko wa pili kwa kasi, tayari tumeshazungumza na wachezaji wetu wasahau matokeo ya mzunguko wa kwanza na sasa waangalie mzunguko wa pili kuhakikisha kila mechi tunapata pointi tatu.
“Tunachoangalia ni kuanza mzunguko wa pili kama vile hatuna pointi, hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kufi kia malengo hayo.
“Mashabiki wanajitahidi kujitokeza sana uwanjani na hata tunapopita njiani, wamekuwa wakituunga mkono, hivyo wachezaji wana deni la kuwalipa ambalo si lingine bali ni kutwaa ubingwa wa ligi kuu.
“Kama uongozi unafanya kazi yake vizuri kuhakikisha tunawapatia wachezaji vitu vyote kwa wakati ili waweze kufanya vizuri na kutwaa ubingwa huo,” amesema Mwakalebela.
Ndani ya Yanga ikiwa imefunga mabao 29, Saido amehusika kwenye jumla ya mabao matano ambapo amefunga mabao mawili na kutoa pasi tatu za mabao.
0 COMMENTS:
Post a Comment