KIPA namba moja wa Klabu ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes, Aishi Manula amesema kuwa watapambana kwa pamoja kufikia malengo ambayo wamejiwekea kutokana na ushirikiano ambao upo kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa imeachwa kwa tofauti ya pointi sita na wapinzani wao Yanga.
Yanga ipo nafasi ya kwanza na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 huku Simba ikiwa na pointi 39 baada ya kucheza mechi 17.
Leo Simba itaibukia Mara kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao wa ligi dhidi ya Biashara United unaotarajiwa kuchezwa Februari 18, Uwanja wa Karume, Mara.
Manula amesema:"Tupo imara na kila mchezaji anatambua kwamba timu inasaka ushindi hivyo ni jukumu letu kuendelea kupambana kusaka ushindi ndani ya uwanja.
"Mashabiki wamekuwa pamoja nasi kila wakati jambo ambalo linatupa nguvu ya kufanya vizuri hivyo tunaamini kwamba tutafanya vizuri," .
Inakutana na Biashara United ambayo inafanya vizuri ndani ya ligi kwa kuwa ipo nafasi ya nne na ina pointi 32 baada ya kucheza mechi 19.
Vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/21 umekuwa na ushindani mkubwa huku Simba wakiwa ni mabingwa watetezi ndani ya ligi.
0 COMMENTS:
Post a Comment