March 7, 2021


 INAKUWA kazi kubwa kwa sasa kufikiria ni nani ambaye atakuwa bingwa wa Ligi ya Wanawake Tanzania kwa sasa kutokana na ushindani ambao upo ndani ya ligi.

Tumeona kwamba kwa sasa ligi imekuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kupambana ndani ya uwanja kusaka ushindi.

Ukija kwa upande wa mashabiki nao wamekuwa na hamasa katika kuzipa sapoti timu zao. Hii ipo wazi ndani ya Ligi ya Wanawake Tanzania. Ubingwa wa ligi ya wanawake ambao upo mikononi mwa Simba Queens bado hauna mwenyewe.

Hiyo inaonekana hasa kwa timu ambazo zinacheza ndani ya uwanja kuonyesha ushindani ikiwa ni mzunguko wa pili. Pongezi mashabiki ambao wanajitokeza kwenye mechi ambazo zinachezwa.

Mchezo wa Yanga Princess na Simba Queens Uwanja wa Uhuru umeweza kutoa picha ya namna ambavyo soka la wanawake linapendwa na linavutia pia.

Kujitokeza kwa wingi kwa mashabiki Uwanja wa Uhuru ni picha kwamba tayari mashabiki wameanza kuelewa kuhusu soka la wanawake.

Mbali na hili pia hata mechi zile za kawaida ikiwa ni pamoja na za kirafiki ambazo zimekuwa zikichezwa kumekuwa na mashabiki ambao wanajitokeza ndani ya uwanja.

Kwa hatua ambayo tupo kwa sasa inamaanisha kwamba mashabiki wanapenda soka. Hivyo mwendelezo wa yale ambayo wanayafanya yasiishie kwenye baadhi ya mechi chache.

Ikiwa watazidi kujitokeza zaidi itafanya maendeleo ya soka letu kwa upande wa wanawake kupiga hatua zaidi ya hapa ambapo tumefika ndani ya ardhi ya Tanzania.

 

Inawezekana kufikia malengo hasa ya kuwa na ligi yenye nguvu na ushindani mkubwa ikiwa maandalizi na sapoti zitaendelea.

Licha ya kwamba mchezo wa soka unapendwa huku wadau wengi walikuwa wamejiweka kando na kuwekeza nguvu nyingi kwa upande wa wanaume.

Kwa namna hali ilivyo na ushindani unavyoendelea ninadhani kwamba itapendeza ikiwa hata wadau nao wakajitokeza kuongeza nguvu upande huu ambao kila iitwapo leo ushindani unakuwa mkubwa.

Kumekuwa na timu chache ambazo zimekuwa na uwezo wa kumudu gharama za uendeshaji, jambo hili nalo litazamwe kwa ukaribu ili kuzifanya timu zote kuwa na nguvu.

Ikiwa kila timu itakuwa na nguvu kwenye uchumi itaongeza hali ya kujiamini kwa timu zote ambazo zinaingia ndani ya uwanja kusaka ushindi.

Yule ambaye atakuwa anarejesha nyuma maendeleo ya soka la Wanawake kwa sasa anapaswa ajiweke kando ili kuruhusu soka letu liendelee kupasua anga.

Kikubwa ambacho mashabiki nao wanapaswa kuendelea kukifanya ni hamasa yao bila ya kuchoka na kukubaliana na matokeo ambayo yanatokea uwanjani.

Imekuwa ni kawaida mashabiki kugoma kukubali matokeo pale ambapo hali inakuwa ngumu kwa matokeo ambayo wanayapata , hilo halipaswi kufuatiliwa.

Muhimu ni kila shabiki kutambua kwamba yale matokeo ambayo wanayapata kwenye ligi ya wanaume hata huku pia ni yaleyale hayajabadilika.

Ndani ya dakika 90 huwa kunakuwa na sare, ushindi na kupoteza hivyo kikubwa ni kukubaliana na hali ya matokeo ambayo yanatokeo ndani ya uwanja.    

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic