June 22, 2021

 


SIMBA sasa ina uhakika wa kumpata kiungo mshambuliaji wa Zanaco, Mzambia, Moses Phiri baada ya meneja mkuu wa timu hiyo, Marlon Kandanda kumuita ofisini kwake na kumtaka wakae kujadili dili hilo.

 

Kiungo huyo ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao, akitumia zaidi mguu wa kulia na fundi wa krosi akicheza winga zote za kulia na kushoto.

 

Kwa mujibu wa Mtandao wa Transfermarkt unaohusika na masuala ya thamani za wachezaji, thamani ya kiungo huyo iliyowekwa mara ya mwisho Juni 29, 2018 ni euro 100,000 ambazo ni sawa na Sh 273,893,000.

 

Dili la kiungo huyo limekuwa rahisi kutua Simba kutokana uwepo wa wakala wa wachezaji watatu wa kimataifa wanaocheza Simba, Mzambia, Paricha Chikoye kuhusika katika kumshawishi bosi wa mchezaji huyo kukubali mteja wake atue Msimbazi licha ya kuwa mipango yao ni kucheza soka Ulaya.

 

Chikoye ni wakala wa kimataifa anayetambulika na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambaye ndiyo amewapa Simba, viungo wa Zambia, Clatous Chama na Rarry Bwalya pamoja na mshambuliaji Chris Mugalu raia wa DR Congo.

 

Mtoa taarifa wetu kutoka Zambia, alisema suala la Phiri kutakiwa na Simba linajulikana kila upande kutokana na uwepo wa Chikoye mwenye uwezo wa kuwashawishi mabosi wa kiungo huyo kukubali dili hilo kutoka Simba.

 

“Suala la Phiri kwenda Simba hadi kufikia Jumapili huenda ikatangazwa rasmi na uongozi wa Zanaco kwa sababu Ijumaa ya wiki hii, Phiri atakutana na meneja mkuu wa Zanaco ili kuweza kujadili juu ya mpango huo wa kwenda Simba ambao pia utahusisha mchezaji wa mkopo.

 

“Mchezaji mwenyewe amekubali kwenda Simba kwa kuwa wakala wa Chama ndiye amehusika katika kumshawishi.

 

"Mikataba ya wachezaji wengi wa hapa Zambia inamalizika Juni, mchezaji huyo naye ni miongoni mwao, hivyo atakutana na huyo bosi siku moja kabla ya mechi ya mwisho ya ligi msimu huu itakayochezwa Jumamosi ijayo,” alisema mtoa taarifa.

 

Takwimu za Phiri msimu huu zinaonesha kwamba, katika mechi 11 alizocheza, amefunga mabao 13, jambo linaloonesha kwamba ni kiungo mwenye kulijua sana goli kama ilivyo kwa Chama na Luis Miquissone ndani ya Simba.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic