June 29, 2021

 

KAMA kuna mtu ambaye bado anawapa watu wengi shida kumuelewa ndani ya soka la Tanzania ni huyu Mghana wa kuitwa, Bernard Morrison.

 

Hii ni kutokana na aina ya maisha ambayo kiungo huyu amejichagulia kuyaishi, maisha ambayo unaweza kuyafananisha na pande mbili za Shilingi.

 

Nje ya uwanja likitajwa jina lake, basi picha ambayo watu wengi wanaipata ni ya mchezaji mwenye matukio mengi ya kukera na kufurahisha, atakukera kama utakuwa hauko upande wake, lakini atakufurahisha kama wewe ni shabiki yake.

 

Sio Yanga tu ambao wanapitia kipindi kigumu kutokana na kero zake kwa sasa, bali nikukumbushe kuwa akiwa Yanga kwa nusu msimu uliopita ni Simba ndiyo walikuwa wahanga wakubwa wa mwamba huyu.

 

Morrison ni mtu ambaye anapenda sana utani kiasi kwamba ni vigumu kujua wapi kuna mstari wa ukomo wa utani wake, mfano mzuri wa hili inaweza kuliona kupitia posti zake za hivi karibuni kumhusu kocha wake Selemani Matola aliposema kipara chake ni kama kioo cha kike.

 

Lakini pia juu ya sakata la Jonas Mkude kutakiwa kwenda hospitali kupimwa kufuatia matukio ya utovu wa nidhamu yanayojirudiarudia, ambapo Morrison amekuwa akiweka machapisho katika mtandao wa Instagram yenye mlengo wa kumtania sana Mkude ambaye ni mshikaji wake mkubwa.

 

Hivi unakumbuka pia kuwa katika mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City baada ya kufanyiwa mabadiliko, Morrison alitoa kituko kingine baada ya kuamua kupumzika katika benchi wachezaji wa akiba wa Mbeya City kabla ya kuja kuondolewa na mwamuzi wa akiba.

 

Licha ya matukio haya ya vituko hasa nje ya uwanja, sura ya pili ya Morrison hasa anapovuka mstari wa kuingia uwanjani ni ya hatari zaidi, huyu ni mwanadamu wa kuhofiwa sana anapokuwa na mpira, hii ni kutokana na uwezo mkubwa wa akili aliyonayo inayoweza kuamrisha mwili wake, kufanya maamuzi yenye madhara makubwa kwa wapinzani.

 

Achana na uhalisia kwamba kwamba, kwa sasa uhusiano wake na kambi ya watani zao wa jadi Yanga kuonekana umezorota, lakini Morrison huyuhuyu ndiye aliyemaliza uteja wa takribani miaka mitano wa Yanga kutopata matokeo ya ushindi mbele ya Simba kufuatia bao lake kali la ‘Mkuki wa sumu’ kwenye dabi ya Kariakoo ya Machi 8, mwaka jana.

 

Lakini unalielezeaje bao lake bora la umbali wa zaidi ya mita 30, dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Mei 29, mwaka huu kwenye uwanja wa Majaliwa?

 

Kama hiyo haitoshi juzi Jumamosi, katika uwanja wa Majimaji Songea, ni akili ya ajabu ya Morrison ndiyo ambayo ilihusika kwa kiasi kikubwa Kuipeleka Simba hatua ya fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho hii ni baada ya kufanyiwa madhambi yaliyoipa nafasi ya kupata bao, huku yeye akiwa amehusika kutoa asisti.

 

“Mnyonge, mnyongeni lakini haki yake mpeni’, licha ya kuwepo mambo mengi kumhusu nje ya uwanja, Morrison anabaki kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa kigeni ambao wamewahi kucheza ndani ya ardhi ya Tanzania.

Uchambuzi wa Acha niseme kwenye gazeti la Championi kila Jumatatu


6 COMMENTS:

  1. Julai 3 atawakera

    ReplyDelete
  2. Alishindwa kuifunga team Kiba ataweza Yanga?
    Watu wamesha msoma awaulize wakina Kondeboy na Chama, siku ya derby watu wanawasahau kama wapo uwanjani

    ReplyDelete
  3. Sawa mtamjua kama vile ulivyosema

    ReplyDelete
  4. Anajua kujidondosha ili apate faulo. Ndio maana alipata kadi kwa marefa wa kimataifa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic