PRESHA kubwa kwa sasa ni kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga unaotarajiwa kuchezwa Julai 3, Uwanja wa Mkapa kutokana na watani hawa wa jadi kuwa kwenye vita ya kusaka pointi tatu.
Kikubwa ni kwamba mashabiki wanahitaji kuona mpira ukichezwa huku ile presha sijui ya timu moja haitaleta timu ikitakiwa kufutwa kwa kuwa timu yenyewe inayotajwa kuwa haitapeleka timu haijatoa taarifa rasmi.
Jambo la msingi kuelekea kwenye mchezo huo kwa sasa kwa Shirikisho la Soka Tanzania ni kuangalia namna gani ratiba yao itakuwa na kuwasiliana pia na Serikali yasije kutokea yale ya Mei 8 ngoma ikabadilishwa wakati mashabiki wapo uwanjani.
Kila kitu kipangwe vizuri na utaratibu uwekwe kwa kuwa nimeona kwa sasa tayari taarifa kuhusu zile tiketi na namna ya kuweza kuingia uwanjani zikiwa zimewekwa wazi.
Kikubwa ambacho kinahitajika kwa mashabiki ambao watajitokeza Uwanja wa Mkapa kuacha kubeba matokeo uwanjani na kuendelea kufanya maandalizi yao kwa hesabu ili kupata pointi tatu.
Kila timu inapaswa kupambana ili kupata kile ambacho kinastahili kwa kuwa jambo la msingi ni kila mchezaji kutimiza jukumu lake uwanjani.
Mashabiki ambao watabeba matokeo mfukoni huwa inakuwa ngumu kwao kuamini kile ambacho watakiona baada ya dk 90 kukamilika hivyo jambo la msingi ni kujiandaa kusubiri matokeo uwanjani.
Ukiweka kando suala la mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga bado kwa sasa ligi ipo kwenye lala salama huku vita ya kushuka daraja ikiwa kwenye kasi yake.
Rai yangu zile ambazo zitashuka zina jukumu la kujipanga upya na kufanya kazi kwa umakini katika kutimiza majukumu yao kwa sababu huku juu ushindani upo na kila timu inahitaji kushiriki ligi.
Wengi wanafuatilia ligi kwa ukaribu na wanajua kwamba kuna ushindani mkubwa hivyo kutambua hilo kwa hao ambao wapo nje ya Dar kunapaswa kuongeza nguvu katika kupambana kwa wachezaji uwanjani.
Hili ni jambo la kujifunza pia kwa wachezaji wetu kuzidi kuonyesha ule uwezo wao wa asili pale wanapopewa nafasi ya kuanza ndani ya timu jambo litakalowaweka sokoni kwa wakati ujao.
Mbali na ligi pia kuna mashindano ya Kombe la Shirikisho na tumeshuhudia robo fainali iliyokuwa na ushindani kwa timu ambazo zilikutana uwanjani.
Azam v Simba ilikuwa ni moja ya mchezo ambao ulikuwa na ubabe mkubwa mwanzo mwisho na soka lilipigwa kwa kila mmoja kushuhudia ushindani mkubwa.
Makosa ambayo waliyafanya Azam FC katika dk za lala salama yaliweza kutoa majibu kwa wapinzani wao Simba kuweza kushinda hii ni kwa mujibu wa nahodha wa Azam FC, Agrey Moriss.
Hatua ya robo fainali ilikuwa inavutia na ni somo kwa timu nyingine ambazo ziliishia hatua za awali kuweza kujipanga katika mechi zao zijazo.
Ukweli ni kwamba mabingwa watetezi wa taji hilo ambao ni Simba wanakwenda kukutana na Yanga waliotinga hatua hiyo kwa ushindi mbele ya Biashara United .
Basi kila timu ijipange vema kwa ajili ya fainali inayotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Lake Tanganyika uliopo Kigoma.
Uzuri ni kwamba kabla ya msimu huu kuanza tuliongea kuhusu mipango ili kuona kwamba namna gani timu inaweza kupata matokeo chanya.
Kwa kilichotokea mwanzo kwa wakati huu hakuna namna ya kubadili zaidi ya kuona kwamba kila mmoja anavuna kile ambacho anakipata.
Kwa timu ambazo zilishindwa kupata matokeo chanya kwenye mechi zao ambazo walicheza iwe ni kwenye Kombe la Shirikisho pamoja na ligi kuendelea kupiga hesabu kali katika mechi zao zijazo.
Kazi kubwa itakuwa kurekebisha yale makosa ambayo waliyafanya wakashindwa kufikia malengo ambayo walikuwa wamejipangia.
Wachezaji ambao walishindwa kuonyesha uwezo wao ni muda wao wa kupata changamoto mpya katika sehemu ambayo inawastahili tofauti na maisha ambayo waliishi wakati uliopita.
Kwenye maisha ya soka kila kitu kinawezekana na mambo kubadilika ni mara moja tu hivyo ikiwa walipata nafasi wakashindwa kuzitumia bado wana nafasi nyingine ya kuonyesha huko ambako watakwenda.
Wapo ambao watakwenda kwenye baadhi ya timu kwa mkopo na wapo ambao watakwenda katika timu zingine kupata changamoto mpya.
Jambo la msingi msimu ujao wakipata nafasi basi wasichezee fursa hiyo kazi yao iwe moja tu kupambana kwa hali na mali kusaka ushindi kwa ajili ya timu zao.
Kila timu ambayo inapabambana kushuka daraja kwa sasa bado ina nafasi ya kushinda mechi zake zilizobaki lakini muhimu ni maandalizi mazuri.
0 COMMENTS:
Post a Comment