LIGI Kuu Tanzania Bara kwa msimu
wa 2020/21 inaelekea ukingoni, ambapo kufikia sasa timu nyingi tayari
zimefanikiwa kucheza michezo 29 au 30 na chache zikiwa na michezo michache ya
hiyo.
Hivyo kwa idadi hiyo ya mechi,
timu nyingi zinasaliwa na michezo minne au mitano tu kutamatisha ligi ya msimu
huu.
Katika hali kama hii, tayari
viongozi wa timu mbalimbali wameanza kuweka nguvu katika mipango ya kuboresha
vikosi vyao kupitia dirisha kubwa la usajili, ambalo linatarajiwa kufunguliwa
mara baada ya kuisha kwa msimu huu.
Kwa kawaida usajili wa dirisha
kubwa huwa mkubwa kwa ajili ya kujenga upya au kuboresha vikosi vya timu
mbalimbali, tofauti na ule wa dirisha dogo ambao ni mahususi kwa ajili ya
kuzisaidia klabu kufanya maboresho ya vikosi vyao, kutokana na tathimini ya
mapungufu ambayo yameonekana katika michezo ya mwanzoni mwa msimu.
Dirisha hili halilengi kuwasaidia
wale tu ambao wamepitia katika kipindi kigumu kwa msimu huu wa 2020/21, bali
hata zile timu ambazo zinakuwa na mpango wa kutwaa ubingwa kwa msimu ujao wa
2021/22, na hata kuanza maandalizi ya michuano ya kimataifa kwa msimu ujao
ambapo tunatarajia kuwa na wawakilishi wanne.
Kwa umuhimu huu, ni wazi kwamba
hakuna anayepaswa kufanya masikhara na kuuchukulia usajili huu kama kichaka cha
mchezo wa bahati nasibu ‘kubeti’, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanajiweka
katika hatari kubwa ya kupoteana kwenye michuano ya msimu ujao.
Mifano mingi kuhusu jambo hili
ipo, kwa uchache tu nawakumbusha kuihusu klabu ya Coastal Union, ambao licha ya
kuwa na kikosi kizuri na mafanikio makubwa msimu uliopita, msimu huu hali yao
imekuwa dhoofu na isiyotabirika.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa
Coastal waliruhusu kuondokewa na wachezaji muhimu, na waliowapa mafanikio msimu
uliopita kama vile aliyekuwa nahodha wao, Bakari Mwamnyeto (Yanga), Ayoub
Lyanga (Azam) na Ibrahim Ame (Simba), huku wakishindwa kufanya usajili mkubwa
wa kuziba mapengo yao.
Coastal hawakuwa pekeyao katika
makosa haya, lakini nimewataja kama mfano ili kuzikumbusha klabu nyingine funzo
hili linalopaswa kuchukuliwa na klabu zote zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao.
Kama kuna timu inajiandaa kufanya
usajili ndani ya kipindi hiki cha dirisha kubwa, inapaswa kwanza wajiridhishe
juu ya tathimini ya mapungufu ya kikosi chao, na pia kukusanya taarifa za
kutosha kuhusiana na nyota wapya wanaotaka kuwasajili ‘scouting’.
Usajili haupaswi kuendeshwa kwa
mihemko kama ambavyo imekuwa ikifanywa mara nyingi na klabu zetu hasa zile
zilizobadilishiwa majina na kuitwa klabu kubwa, ambao imefika wakati husajili
mchezaji eti kwa sababu alitajwa kuwa na uelekeo wa mpinzani wake.
Hali hii humpa wakati mgumu kocha
kutokana na kuwa na rundo la wachezaji ambao hakuwapendekeza, na ambao
hawakidhi matakwa yake kiasi cha kuwasotesha benchi.
Kama ni kweli tunahitaji maendeleo basi ni lazima tuhakikishe tunaondokana na tabia za kufanya mambo kwa kubahatisha kwani mtazamo huu hauna afya chanya kwa soka letu.
Uchambuzi wa Edibily Lunyamila, unaweza kuusoma uchambuzi huu kupitia gazeti la michezo la Championi Jumatatu, linalotoka kila Jumatatu.
0 COMMENTS:
Post a Comment