LEGEND legend legend haswaa, Didier Drogba ni moja ya mastaa ambao rekodi zao zinaishi kila wakati kutokana na makubwa ambayo alikuwa akiyafanya ndani ya uwanja.
Ni mzaliwa wa Abidjan, huko Ivory Coast urefu wake ni m 1.88 nafasi ambayo anaimudu kuicheza bila bugudha ni ile ya ushambuliaji.
Katika timu ya taifa ya Ivory Coast alikuwa ni nahodha wa muda wote kuanzia 2006 mpaka 2014 alipostaafu na anashikilia rekodi ya kuwa nyota mwenye mabao mengi ndani ya timu ya taifa ambayo ni 65.
2006 anakumbukwa kwa kukiongoza kikosi cha timu ya taifa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia na alicheza jumla ya mechi 105 katika timu ya taifa ya Ivory Coast.
Alikuwa kwenye kikosi cha timu yake ambacho kilitinga hatua ya fainali ya Afcon ilikuwa 2006 na 2012 lakini zote fainali alishuhudia timu yake ikinyooshwa kwa penalti. Alitangaza kuacha majukumu katika timu ya taifa Agosti 2014 na aliachana na soka la ushindani 2018.
Aliletwa duniani Machi 11, 1978 kwa sasa ana umri wa miaka 43. Ndani ya Ligi Kuu England alicheza jumla ya mechi 254 alifunga mabao 104 na pasi za mabao 64.
Jumla alicheza mechi 686 na alifunga mabao 300 akiwa na pasi za mabao ambazo ni 126. Tuzo mbili za mchezaji bora wa Afrika ilikuwa ni 2009 na 2006 wakati anakipiga Chelsea, tuzo ya ufungaji bora mara nne, mara mbili katika Ligi Kuu England mara moja UEFA na mara moja Afcon.
Mataji manne ya English Champion, taji moja la Champions League, mataji manne ya FA, mataji matatu ya English League Cup, mataji manne ya English Super Cup na yote haya aliyatwaa akiwa na Chelsea ni sehemu ya mafanikio ya mwamba huyu.
0 COMMENTS:
Post a Comment