JOTO limeanza kupanda taratibu kuelekea kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga v Simba unaoatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Septemba 25.
Timu zote mbili zimeonja ladha ya kambi ya nchini Morocco ambapo Simba wao walitangulia na kwa sasa bado baadhi ya wachezaji wamebaki nchini Morocco huku wale wa Yanga wote wakitarajiwa kurejea Dar leo.
Kwa muda ambao wamekaa kambini imeonekana timu kuanza kupata munganiko kabla ya kusitisha kambi hiyo ambayo awali ilikuwa inatajwa kuwa ingekuwa ni ya muda wa siku 10.
Timu ya Simba yenyewe licha ya kuwa pungufu imeweka wazi kwamba itaendelea na wale ambao wamebaki kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2021/22.
Wakati wa maandalizi ya msimu mpya Simba ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya FAr Rabat ya Morocco na ngoma ilikamilika kwa timu hizo kutoshana nguvu ya kufungana mabao 2-2.
Kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi pia mbali na mchezo huo wa Ngao ya Jamii kina kazi pia ya kupambana kwenye mashindano ya kimataifa ambapo kitakuwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa Fredrick Mwakalebela, Makamu Mwenyekiti wa Yanga ameweka wazi kwamba kila mchezaji yupo tayari kwa ajili ya msimu mpya na wanaamini kwamba watafanya vizuri.
Kwa mujibu wa Meneja wa Simba, Patrcik Rweyemamu, amesema kuwa maandalizi yanakwenda vizuri na wanaamini kwamba watafanya vizuri msimu ujao.
Kwa miaka minne mfululizo, Simba iliweza kufanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii kwenye mechi ambazo walicheza jambo ambalo linaongeza ushindani kuelekea kwenye mchezo huo ambao unasubiriwa kwa shauku na mashabiki.
0 COMMENTS:
Post a Comment