KUELEKEA mchezo wao ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi Pyramid kutokea Misri, uongozi wa Azam FC umetamba kuwa unatambua ubora wa wapinzani wao, lakini upo tayari kwa ajili ya kupambana kwenye mchezo huo.
Azam wanatarajiwa kuvaana na Pyramid Oktoba 16, mwaka huu katika mchezo wa hatua ya kwanza ya michuano hiyo ambapo wataanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.
Katika hatua ya awali Azam iliwaondosha Horseed ya Somalia kwa jumla ya mabao 4-1, wakishinda mabao 3-1 mchezo wa kwanza na bao 1-0 waliporudiana.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Azam, Zakaria Thabith alisema: “Sehemu ya wachezaji ambao hawajaitwa kwenye vikosi vya timu zao za taifa inaendelea na mazoezi yaliyoanza tangu Jumanne wiki hii, ili kujiandaa na ratiba ya michezo iliyo mbele yetu.
“Mchezo wetu ujao ni ule wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramid FC ya Misri. Kocha mkuu George Lwandamina anajua ubora wa wapinzani wetu lakini nasi tunajiamini na tupo tayari kupambana kuiwakilisha vyema nchi yetu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment