April 19, 2014

 
NORWICH CITY WAKISHANGILIA MOJA YA MABAO YAO
Na Saleh Ally
KUANZIA leo, kesho na keshokutwa utakuwa ni mtihani mkubwa kwa timu zinazowania ubingwa kwa kuwa zinakutana na timu ambazo lazima zishinde au hazina cha kupoteza.

Timu zinazopambana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England ni Liverpool, Manchester City na Chelsea huku ikionekana Arsenal wamebaki kwenye zile mbio zao za kila msimu, kuwania kupata nafasi katika nne bora ili washiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini hao wanaopambana kupata ubingwa, wiki hii wana mechi ambazo mwendo wake unaonyesha lazima kunaweza kutokea kwa hali ya kushangaza hasa kama hawatakuwa makini.
Takwimu za Ligi Kuu England maarufu kama Premiership inaonyesha hivi, timu zinazokuwa kwenye hatari ya kuporomoka daraja, zimekuwa ni msumari kwa kuwa zimekuwa zikizikosesha ubingwa timu zilizo juu kwa asilimia 69.
STOKE KAZINI KUIZUIA CHELSEA..

Wakati zile timu ambazo ziko katika hali ya kutokosa lolote, kwamba hazitateremka daraja au kuchukua ubingwa, nazo zimezikosesha zile zilizokuwa zinawania ubingwa nafasi hiyo kwa asilimia 54.
Hivyo timu ambazo zinawania kuepuka kuteremka daraja ndizo hatari sana kwa timu zinazotaka kuwa bingwa na ratiba ya leo, kesho Jumapili na keshokutwa Jumatatu zinaonyesha Chelsea, Man City, Liverpool na Arsenal zitakuwa na wabishi hao.
Timu zinazokaribia kuteremka daraja ambazo zinapambana kuepuka kuanguka, kawaida zimekuwa zikiongeza kiwango kwa zaidi ya asilimia mia katika mechi zao nane za mwisho za msimu.
Hivyo kukutana na timu ambayo inakaribia kuteremka daraja, wakati unapambana kupata ubingwa, mechi inakuwa na presha mara mbili zaidi ya kawaida.

JUMAMOSI:
Chelsea Vs Sunderland
Katika mechi nane za mwisho, Chelsea bado ina rekodi nzuri kwa kuwa imeshinda sita na kupoteza mbili tu. Hivyo ni ya kiwango cha juu kama utailinganisha na Sunderland ambayo inashikilia mkia, imetoka sare mbili na kupoteza sita zilizobaki.

Lakini hapo ndiyo utajua maana ya mchezo wa soka kuwa na mashabiki wengi zaidi kwa kuwa hautabiriki hata kidogo, kwani Sunderland tayari imeitoa Man City ‘jasho la meno’ baada ya vijana hao wa Manuel Pellegrini kujikuta wanapambana kusawazisha.
Sunderland wana pointi 26 wakiwa wamebeba timu zote 19, lakini bado wanaamini wanaweza kuokoka na wanataka kushinda. Chelsea wana 75 katika nafasi ya pili, wanajua wakiteleza mechi moja, wataiachia njia Man City kwenda kupambana na Liverpool.
Vijana hao wa Jose Mourinho wanataka kuendelea kutopoteza nyumbani, hivyo ni vita isiyokuwa na mwenyewe.


JUMAPILI:
Hull City Vs Arsenal:
Unaweza kusema ni mechi ya majaribio ya fainali ya Kombe la FA. Maana hizi ndiyo timu zitakazocheza siku hiyo, lakini safari hii ni mawazo tofauti kabisa kwa kuwa Arsenal wanataka nafasi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Hull City, hawana cha kupoteza lakini wanatakiwa kushinda na kujiweka vizuri kwa kuwa pointi 36, haziwahakikishii kwa asilimia kubaki.
Itakuwa mechi ngumu kwa kuwa Hull City waliopoteza mechi mbili kabla, waliibuka na kushinda, hivyo ni lazima wajihakikishie nafasi ya kubaki.

Norwich Vs Liverpool:
Norwich wana pointi 32, wakichezea nafasi wameumia na Liverpool wanajua wakikosea, basi Chelsea na Man City watawadhuru, hivyo hakuna utani.
Norwich wamepoteza mechi zao zote tatu za mwisho, lakini wanajua matumaini yao yanaweza kupatikana kupitia vijana hao wa Anfield ambao watakuwa wageni wao kesho.

JUMATATU:
Man City Vs Wes Brom
Man City wana hofu kwa kuwa mechi yao ya mwisho wamelazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Sunderland wakiwa wametoka kupigwa mabao 3-2 dhidi ya Liverpool.
Wes Brom wanajulikana kwa ubishi, hakutakuwa na utani kwa kuwa mechi yao ya mwisho walitoka sare na wenyewe wanataka kubaki ligi kuu kwa kuwa wana pointi 33.
Maana yake itakuwa ni vita ya anayetaka kubaki na aliyepania kuchukua kombe, si kazi Rahisi. Hata hivyo Wes Brom hawana rekodi nzuri ya ugenini kwa kuwa katika mechi 16, wameshinda tatu tu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic