UKIZUNGUMZIA suala la uwezo uwanjani kwa
mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, haliwezi kuwa suala lenye maswali mengi
kwa kuwa jibu lake litapatikana kwa urahisi sana.
Okwi ana uwezo mkubwa, achana na zile taarifa
za kwamba amekwisha, Okwi wa mwaka jana si wa mwaka huu au vinginevyo. Mchezaji
anaweza kuamua awe katika kiwango kipi na wakati upi.
Inajulikana vitu vipi vinavyoweza kumfanya
mchezaji awe bora, hili pia litakuwa linamhusu Okwi na hakika haliwezi kuwa
jambo geni kwake, kwamba amelisikia jana.
Lazima mchezaji afanye mazoezi ya kutosha
ambayo yamepangiliwa kitaalamu, ndiyo maana klabu zinaajiri makocha bora kwa
ajili ya timu zao.
Baada ya kazi ya kocha, mchezaji ndiye
anatakiwa kujilinda ili kuhifadhi mazoezi aliyopewa na mwalimu au walimu wake.
Kuna mambo anatakiwa asifanye ili aendelee kubaki fiti.
Suala la starehe hakuna haja ya kuficha,
ngono, uvutaji sigara, ulevi kupindukia na kutojipatia muda wa kutosha wa
kupumzika ni tatizo.
Iwapo mchezaji hatafanya mazoezi halafu atake
kung’ara ni kichekesho au afanye mazoezi halafu ashindwe kujitunza ni
kichekesho kingine.
Hivyo, Okwi pamoja na kwamba ana kipaji,
lakini lazima ajue kuwa anatakiwa kuwa makini na hayo niliyoyaeleza na hakuna
ubishi akifikia hivyo na kwa kipaji alichonacho, basi ana uwezo wa kusumbua
hapa nchini na nje ya mipaka.
Maana ya kueleza haya ni kwamba, suala la
kusema Okwi amekwisha ni lake, anaweza kuamua asiwe hivyo au awe hivyo. Yeye
ndiye mwenye uamuzi wa mwisho.
Kilichonivuta kuandika Hoja Yangu leo ni suala
la mashabiki. Wale wa Yanga ambao wana hasira naye kwa kuwa ana mgogoro na
klabu yao, wamekuwa wakimbeza lakini kitu kizuri hakuna anayemtupia kashfa
zaidi ya ule utani wa watani wa jadi.
Msemo wa “Okwi mwisho Chalinze, mjini kila mtu
Jaja” umezagaa kwa kasi ya kimondo katika mitandao mbalimbali hadi vyombo
vingine vya habari, hali iliyosababisha Okwi naye kujibu mapigo kupitia Mtandao
wa Kijamii wa Facebook.
Okwi ameapa kwamba wanaomdharau, siku itafika
na watafuta msemo huo. Ni jambo zuri kwa kuwa analenga kufanya vizuri, lakini
kuna mambo muhimu ya kuangalia kwake.
Wachezaji hawawezi kufurahi kucheza mechi bila
ya mashabiki na timu haina maana kama itakuwa inacheza na mashabiki wake tu
uwanjani. Ndiyo maana nataka kumsisitizia Okwi kuwa, atambue kuwa mashabiki
wapo nao ni familia ya mpira.
Wanasema nini kuhusu wachezaji au yeye, hilo
ni suala jingine ila wana haki ya kuanika hisia zao na mfumo wao unapishana na
mfumo wa wachezaji lakini mwisho vyote viko ndani ya mpira.
Mashabiki watakuwepo tu na Okwi hapaswi
kupania kucheza vizuri zaidi kwa ajili yao. Kuna mawili, anaweza kufanikiwa au
kufeli na kauli yake ya kwenye Facebook inajenga dalili zote kwamba ‘amepaniki’.
Akiendelea hivyo, itazidi kumfanya ‘apaniki’,
badala yake anatakiwa kuonyesha kweli yeye ni ‘professional’, aelekeze nguvu
zake uwanjani badala ya jukwaani. Kwani kama masikio yake yatakuwa jukwaani
badala ya uwanjani, atafeli.
Wachezaji walioweka nguvu zao nyingi kwenye
ushindi uwanjani, huwa hawana habari na mashabiki, hawahitaji kuzungumza kuhusu
wao na badala yake ni vitendo tu.
Kutoa hisia ni jambo zuri, unaweza pia kusema
alichokifanya Okwi si kibaya sana. Lakini pia anatakiwa kutotupia nguvu nyingi
walipo mashabiki na badala yake nguvu uwanjani na malengo ya kufanikiwa.
Bado Okwi ana nafasi ya kufanya vema kuliko
wengine wanavyoamini. Haina ubishi, kuwa makini zaidi na malengo ya mafanikio,
ndivyo vitakavyomfanya ashinde vita dhidi ya wanaotaka afeli.
0 COMMENTS:
Post a Comment