May 7, 2015

ADEBAYOR AKIWA NA MAMA YAKE...
ULIWAHI kusikia mshambuliaji Emmanuel Adebayor amemfukuza mama yake mzazi kwenye jumba lake la kifahari?


Adebayor raia wa Togo na fowadi wa zamani wa Arsenal amekuwa akikanusha hilo. Amekuwa akidai kuna matatizo lukuki ndani ya familia yake.

Hivi karibuni alikwenda kuomba ushauri kwa mshambuliaji wa Chelsea, Didier Drogba kuhusiana na suala hilo ambaye alimshauri kuishi anavyoona ni sahihi si kuangalia watu wanataka nini.

Kama hiyo haitoshi, kupitia mtandao wa FaceBook, Adebayor aliamua kuweka hadithi  nzima kuhusiana na matatizo yake kwenye mtandao wa Facebook

Jamaa amefunguka vilivyo na hii ndiyo barua aliyotupia kwenye mtandao huo wa kijamii akieleza kila kitu kuhusiana na mama yake, dada na kaka zake na kila kitu kilivyo.

Hakika inatia huzuni na kama kila kitu alichoweka ni sahihi, huenda ikawa funzo kwa wanamichezo na wanasoka wa Tanzania. Inachanganya ila anza kuisoma sasa.

“Niliamua kuihifadhi hii stori kwa muda mrefu sana, lakini leo nimeamua kufunguka kuhusiana na haya matatizo ya kifamilia ambayo yamekuwa yakinikabiri.

“Kweli matatizo ya kifamilia hayawezi kutatuliwa hadharani hivi, lakini nimeamua kufanya hivi huenda wengine wanaweza kujifunza kupitia kilichonitokea.

“Nikiwa na umri wa miaka 17, ikiwa ni ajira yangu ya kwanza kama mwansoka, niliijengea familia yangu nyumba nikitaka kuhakikisha wako.

“Unakumbuka nilipotangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika mwaka 2008, nilimpandisha mama yangu kwenye steji ili kumshukuru. Mwaka huohuo nilimsafirisha hadi London kwa ajili ya matibabu.

“Alipozaliwa binti yangu, tulimpigia mama kumpa taarifa hiyo njema. Lakini ajabu alikata simu haraka na hakutaka kusikia lolote kuhusiana na hilo! Unakumbuka, wakati fulani watu waliwahi kushauri kwamba kutokana na matatizo yetu ya kifamilia tungewasiliana na TB Joshua.


Mwaka 2013, nilimpa mama fedha, ili asafiri hadi Nigeria na kukutana na TB Joshua. Alitakiwa kukaa wiki moja, lakini nilitaarifiwa kwamba aliondoka Nigeria baada ya siku mbili tu! Achana na hilo, nilitoa fedha nyingi nikampa mama ili aanzishe biashara ya biskuti.


“Pia nikawaruhusu kutumia picha na jila langu ili waweze kuuza kwa wingi biskuti hizo. Sasa nini hapo mtoto anaweza kufanya zaidi ya hapo ili kuisaidia familia yake?

“Miaka kadhaa iliyopita, nilinunua nyumba nchini Ghana, thamani yake ni dola milioni 1.2. Niliona kawaida kumuacha dada yangu aishi pale. Pia nilimruhusu Daniel ambaye ni mdogo wangu kwa upande wa mzazi mmoja naye aishi pale.

“Miezi michache baadaye, nilishangazwa baada ya kugundua dada yangu aliipangisha nyumba ile na pia kumtimua Daniel! Nyumba hiyo yenye vyumba 15 sasa ilikuwa na wapangaji, nilipompigia dada yangu kutaka kujua nini tatizo baada ya mimi kwenda kwenye nyumba hiyo wakati wa kipindi cha likizo na kukuta lundo la magari ya wapangaji, alinitukana kwa takribani nusu saa.

“Niliona lingekuwa jambo zuri kuwasiliana na mama na kumuelezea hilo. ajabu naye aliungana na dada yangu akitumia muda kama ule akiniporomoshea matusi na maneno makali.


“Pamoja na maneno ya kashfa nilionekana siisaidii familia. Lakini nikahoji hata gari anayoendesha ni mimi ndiye nilimnunulia.

“Hiyo ni kidogo, kaka yangu Kola Adebayor, sasa ameishi nchini Ujerumani kwa miaka 25. Anasafiri kurudi nyumbani kusalimia karibu mara nn kwa mwaka kwa gharama amabzo nalipa mimi. Nalipa gharama zote za shule kwa watoto wake.

“Nakumbuka aliwahi kuja hadi Monaco wakati nikiwa huko na kuniomba mtaji wa biashara. Mungu ndiye anayejua kiasi cha fedha nilichompa. Leo biashara yenyewe iko wapi? Lakini alipofariki kaka yangu Peter, huyu Kola akasema mimi ndiye ninahusika na kifo chake! Kivipi?

“Kola ndiye aliyekwenda katika gazeti la The Sun kuuza stori ili apate fedha. Kwa pamoja, familia yangu walituma barua kwenye klabu yangu wakati nikiwa Real Madrid kwamba nifukuzwe.

“Nikiwa Monaco pia, nilipenda kuona familia yangu ina wanasoka wengine waliofanikiwa. Nikajitahidi kuhakikisha mdogo wangu Rotimi anapata nafasi kwenye moja za akademi bora za nchini Ufaransa.

“Unaweza ukaona kama miujiza, kwani katika miezi michache tu, ndugu yangu huyo wa damu alikuwa ameiba simu za wachezaji 21 kati ya 27 wa akademi aliyekuwepo!

“Siwezi kusema chochote kuhusiana na kaka yangu Peter kwa sababu ameishatangulia mbele ya haki. Lakini dada yangu Lucia Adebayor amekuwa akilazimisha nimlete Ulaya kwa madai baba yangu alisisitiza nifanye hivyo. Nikimuuliza kwa nini, anasisitiza kwa kuwa tu anataka kuja. Ulaya watu wako kwa sababu maalum!

“'Nilikuwa Ghana, nikapata taarifa za ugonjwa wa Peter ambaye alikuwa taabani, nikaamua kuendesha gari kwa kasi kubwa kwa lengo la kumuona na kusaidia pia.

“Nilipowasili Togo mama akaniambia wala nisingekwenda, ningetuma fedha tu yeye angeshughulikia kila kitu. Mungu ndiye anajua nilimpa kiasi gani cha fedha.

“Nilifanya hivyo ili kumsaidia kaka yangu, leo watu wanasema sikufanya lolote kumsaidia Peter. Kweli ningeweza kuendesha kwa masaa mawili tena kwa mwendo kasi kwenda Togo?

“Mwaka 2005, nikaitisha mkutano wa familia ili tuweze kumaliza matatizo yetu. Nilipowauliza kuhusiana na mawazo yao kuwa nini cha kufanya, wakashauri kuwa niwanunulie ndugu wote nyumba ikiwa ni pamoja na kuwalipa mshahara!

“Leo nikiwa hai, tayari wamegawana vitu vyangu utadhani niliishakufa. Imechukua kipindi kirefu kwangu kufanikisha kusimama kwa foundation yangu. Hii ni kwa kuwa wote hawakukubaliana na wazo langu la kusaidia watu wengine wakiona halikuwa sahihi.

“Siandiki hili kwa ajili ya kuwavua nguo wana familia kutoka katika familia yangu. Lengo ni wengine wenye familia zao hasa kutoka Afrika wajifunze kupitia yaliyonitokea.”

EMMANUEL ADEBAYOR




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic