August 3, 2015


Na Saleh Ally
MICHUANO ya Kombe la Kagame imemalizika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku kukiwa na mengi ya kufurahia na kujifunza.
Kwanza ilikuwa ni Watanzania kuona timu yao angalau moja inaingia fainali kulinda heshima na baadaye ikiwezekana kuhakikisha inabeba kombe.
Ingawa Yanga ndiyo ilipewa nafasi zaidi, safari yake ikaishia robo fainali na Azam FC ikasonga hadi kukutana na Gor Mahia ya Kenya ambayo imebeba kombe hilo mara tano tangu ikijulikana kama Luo Union au Luo Star.
Hongera kwa Azam FC kwa kuiwakilisha vyema Tanzania, wachezaji wake, makocha, viongozi wamefanya kazi yao. Wanastahili pongezi, lakini pongezi zaidi ni kwa wamiliki ambao wamebadilisha mambo mengi ambayo huenda yalionekana yasingewezekana hapo awali.
Si rahisi kutaka kufikia mafanikio angalau robo ya yale ya Real Madrid, Barcelona au Manchester United wakati ndoto zitaendelea kubaki zilezile za kuamini ‘komandoo’ ndiye mwenye nguvu hata kuliko mwenyekiti wa timu.
Timu kubwa za Ulaya au hata zile kubwa na maarufu za Afrika kama Al Ahly, Zamalek au TP Mazembe hazikufikia hapo kwa ndoto, yaani wahusika wakiwa wamelala tu na mambo yakaenda.
Wakati kila kitu cha Azam FC kikienda, tena ikiwa haijafungwa hata bao moja hadi inafika fainali, gumzo kubwa lilikuwa ni beki Serge Pascal Wawa raia wa Ivory Coast.
Wawa amekuwa gumzo, Kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee amefikia kumfananisha na mwanajeshi. Akieleza kama asingecheza soka, basi angekuwa ni mwanajeshi.
Kweli, Wawa amecheza vizuri sana michuano hiyo na amekuwa kiongozi wa wenzake uwanjani kuhakikisha kila kitu kinaenda bomba. Alikuwa shujaa hadi mwisho wa michuano.
Uchezaji wa Wawa, umezua maswali na Watanzania wapenda soka wameanza kuhoji hivi; “Kama kweli Wawa ndiyo hana nafasi kwenye timu ya Ivory Coast, kwa uwezo wake, basi lazima tujipange maana Tanzania hapa angekuwa tegemeo.”
Si swali baya kujiuliza ingawa kwa kuwa wachezaji wetu wengi wamekuwa wakishuka viwango na kuwafanya wale wa zamani wabaki kuwa bora zaidi.
Kwa mimi niliyebahatika kumuona Salum Kabunda ‘Ninja’ au Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, Mustapha Hoza, hakika sioni kinachonishangaza kwa Wawa badala yake nitasifia kweli ni mchezaji mzuri.
Wawa si mchezaji ambaye Tanzania haijawahi kuwa naye katika safu ya ulinzi. Ni mchezaji ambaye si mzuri kuliko wote ambao Tanzania imewahi kuwa nao. Lakini ninakubali wengi wa wachezaji wa sasa wanaweza wasiwe na kiwango chake na sasa ndiyo wakati wa kujipima na kuangalia walipo ndiyo mwisho.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ni kati ya mabeki bora kabisa ambao tumekuwa nao, bado nampa nafasi ya mmoja wa mabeki bora ambao wana uwezo wa kuongoza wenzao, wanajituma na wanapambana kwa ajili ya timu, wako tayari kwa lolote.
Wawa anaweza asiwe na ubora wa kutisha, lakini moyo wa kutaka kushinda, kutokukubali kushindwa, kupambana kwa ajili ya klabu yake na maisha yake ndiyo jambo linalomfanya aonekane bora kweli.
Usisahau kabla ya kutua Azam FC ametokea katika moja timu kubwa barani Afrika ya El Merrekh ya Sudan. Si mtu anayebahatisha lakini anapigana kweli kwa ajili ya mafanikio na inakuwa si rahisi hata akiomba kuongezewa mshahara katika mkataba mpya, mwajiri akasema hapana.
Wachezaji wetu wanalewa sifa mapema, waoga wasiokubali changamoto, wanaohofia kutoka nje ya nchi yao. Wanalewa sifa za nyumbani na kujiona wamefika mapema. Lakini wakijituma kweli na kwa malengo, basi aina ya Wawa wako rundo hadi watamwagikia.
Wawa hana nafasi kwenye kikosi cha Ivory Coast kwa kuwa yeye ni kati ya wachezaji 500,000 wa nchi yake wanaojituma, wanaotaka kushinda kitimu na kufanikiwa kimaisha.
Ushindani uko juu, Wawa anaujua, ndiyo maana anapambana. Hapa nyumbani, wachezaji wanaamini kuwa Yanga au Simba ndicho kigezo cha kucheza timu ya taifa. Mgeuzeni Wawa awe ubao, chaki mkononi mwenu, mpige hesabu, majibu mtabaki nayo wenyewe.



                       


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic