Na Saleh Ally aliyekuwa Cairo
MAKALA haya yalianza jana wakati nilipoelezea hali iliyojitokeza katika kambi ya Taifa Stars jijini Cairo, Misri timu ikiwa huko kushiriki michuano ya Afcon.
Hakuwa na uelewano mzuri kati ya wachezaji pamoja na Kocha Emmanuel Amunike na hasa baada ya kocha huyo raia wa Nigeria kuendelea kuwatukana wachezaji akiwaeleza maneno makali akiwafananisha na wanawake.
Nilianza kueleza namna Amunike alimvyomwita Yondani kuwa anacheza kama wanawake. Jambo ambalo lilimfanya beki huyo kuanza kulia.
Kumbuka wakati huo ulikuwa ni ule wa mapumziko kabla ya kurejea dakika 45 za mwisho kumalizana na Kenya. Kama unakumbuka Taifa Stars ilikuwa inaongoza dhidi ya Wakenya.
Jana tuliishia pale baadhi ya wachezaji kuanza kumbembeleza Kelvin Yondani baada ya Kocha Emmanuel Amunike kumuambia anacheza soka kama mwanamke.
Yondani alianza kumwaga chozi kutokana na maneno makali ya kocha huyo ambaye imekuwa ni kawaida yake kuwakashifu wachezaji wa Stars katika michuano mbalimbali waliyoshiriki.
Pamoja na wachezaji wengine kujaribu kumbembeleza Yondani, mambo yalishindikana. Ilionekana alichukua uamuzi wa kupumzika na kuwapa nafasi wengine wacheze ambao kocha angeweza kuwaona wanacheza kiume.
Nahodha, Mbwana Samatta naye aliingilia na kumchukua Yondani pembeni, wakazungumza akimshawishi na kumkumbusha walikuwa wakipigania taifa lao.
Samatta aliwaunganisha wachezaji wengine na kuwaambia ulikuwa ni wakati mzuri wa kuungana pamoja kwa ajili ya taifa na kusahau mengine yote yaliyokuwa yametokea katika kipindi hicho.
Wachezaji walionekana kumsikiliza Samatta na wengine waliendelea kumpoza Yondani ambaye hakika alionekana kuwa na hasira sana.
“Haikuwa hali nzuri, muda wote wa vyumbani haukuwa na faida hata kidogo. Unajua wachezaji (wa Stars) wakati wanarejea uwanjani hawakuwa wamezungumza au kuchukua jambo lolote kwa kocha kwa ajili ya kipindi cha pili.
“Kipindi chote cha mapumziko kiliisha kwa malumbano na kelele za ajabu utafikiri Kenya ndiyo walikuwa wanaongoza dhidi ya Tanzania. Hii inawezekana ilitoa nafasi kwa Kenya kusawazisha,” kilieleza chanzo cha uhakika kilichokuwa chumbani wakati wa timbwili hilo.
Wachezaji walirejea uwanjani na ndipo Kenya ikafanikiwa kusawazisha na kufunga la tatu. Jambo ambalo liliifanya taifa Stars kupoteza mechi yake ya pili na kuwa imepoteza kabisa matumaini ya kucheza Hatua ya 16 Bora ya Afcon.
Kwa kifupi, Stars ikawa ndiyo imefungashiwa virago na mechi ya mwisho ilikuwa ni dhidi ya Algeria waliokuwa wanaonekana wako vizuri zaidi maana tayari walishinda mechi zao zote za kundi dhidi ya Senegal pia Kenya.
Tangu kumalizika kwa mechi ya Kenya, kambini hakukuwa kumetulia ingawa kwa mwonekano wa kawaida, mambo yalionekana kama yamepoa.
Wachezaji wa Taifa Stars waliendelea na mazoezi na juhudi zilikuwa juu kupitia mawazo ya Samatta kwamba walikuwa wakipambana kwa ajili ya taifa lao.
Kumbuka tayari Amunike alishakuwa ametengeneza jambo lililozua tafrani kati ya wachezaji na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Amunike aliamua kwenda kuwatangazia wachezaji posho imepanda kutoka dola 75 (zaidi ya Sh 172,000) hadi dola 300 (zaidi ya Sh 688,000).
Uamuzi wake wa kuwaambia wachezaji bila ya kuwashirikisha viongozi wa TFF, ilizua hali ya kutoelewana tokea awali. Hali hii ililalamikiwa sana na viongozi wa shirikisho hilo.
“Kocha alituvuruga, unajua hakuwa na uhusiano mzuri na wachezaji akaamua ghafla kusema wapewe dola 300 akijua haikuwa sahihi na TFF haina uwezo huo.
“Angekuwa anataka wachezaji waongezewe fedha kwa nia njema, basi angewasiliana na TFF kwanza ili wamweleze lakini hakufanya hivyo,” kilieleza chanzo kingine ambacho kinaamini alifanya hivyo kwa nia ya kurejesha imani ya wachezaji kwake, bila ya kujali anawachonganisha TFF.
Kilichofuata baada ya hapo, TFF walifanya kazi ya ziada kuzungumza na wachezaji na kuwaeleza hali halisi. Lakini kiongozi mmoja wa TFF inaelezwa alimtolea uvivu Amunike na kumueleza alichofanya hakikuwa sahihi kwa kuwa anavunja morali ya wachezaji na pia kuwachonganisha na shirikisho hilo.
Tayari hapo hali ya sintofahamu ilishaanza kuingia na mwisho unaona kuna wachezaji kama Yondani wakaeleza kuumia na kukaa nje kama ilivyokuwa kwa kipa Aishi Manula.
Usisahau wakati wanakaa nje katika mechi ya mwisho dhidi ya Algeria, wachezaji wawili, Yondani na Erasto Nyoni baada ya timu kushuka Dar es Salaam, walitangaza kustaafu.
Inawezekana suala la vurugu wakati wa Afcon zilichangia wao kuchukua uamuzi huo na unaona wakongwe ndiyo wamechukua uamuzi huo kwa kuwa matarajio yao makubwa yalikuwa ni heshima badala ya dharau na kufananishwa kuwa dhaifu kama wanawake.
Hakuna anayetamka hadharani lakini hali ya maelewano kati ya Amunike na wachezaji wengi wa Stars haiko vizuri. Lakini bado kuna viongozi wa TFF wameendelea kubeba mzigo katika vifua vyao kwa hofu ya suala la kuhusiana na Amunike, jambo ambalo baadaye litakuwa tatizo kubwa.
Yondani ameingia katika rekodi ya kutukanwa na Amunike, lakini kuna wengine wawili, Abdi Banda ambaye inaelezwa pia aliitwa mwanamke, akashindwa kuvumilia na kuamua kumjibu kocha huyo, jambo ambalo limesababishha hali ya kutoelewana hadi leo.
“Banda yeye alionyesha ‘action’ wakati huohuo, kwanza alimkataza kocha kumuita kama mwanamke lakini alipoona anasisitiza, alichofanya ni kumjibu na kumrudishia. Hili lilimkera kocha, kama unakumbuka hata mechi dhidi ya Lesotho hakumuita,” kilieleza chanzo kingine.
Zaidi ya wachezaji wanne waliofanya mahojiano nami, wanaeleza kutokukubaliana na Amunike hasa aina yake ya umwagaji matusi lakini hali ya kuwakatisha tamaa.
“Sisi tumekuwa tukielewa zaidi mafunzo ya wale makocha raia wa Misri ambao waliongezwa baada ya kutua hapa Misri. Lakini kocha anachanganya sana, wakati mwingine haujui hata anataka nini. Bahati mbaya ukikosea kidogo tu anakuita kama mwanamke, inatuumiza sana,” anaelezea.
Siku moja kabla ya mechi dhidi ya Algeria, hii ndiyo ilikuwa ni funga mwaka baada ya kijana mmoja ambaye anajulikana kuwa ni wakala wa kocha huyo kutua katika kambi ya Stars akiwa na nia ya kuona timu inafungwa mabao mengi.
Mmoja wa maofisa wa TFF amemrekodi mtu huyo wakati akishawishi suala la matokeo. Alitaka Stars ifungwe mabao mengi, hali ambayo imezua mjadala mkubwa wengine wakiamini kwamba kuna suala la kamari.
Ndani ya shirikisho hilo, hali hiyo imezua taharuki kwamba vipi Mwarabu huyo wa Misri atengeneze ushawishi huo? Anataka nini na kama ni wakala wa kocha, vipi anafanya hivyo na kocha atakuwa halijui hilo?
MECHI ZA TAIFA STARS AFCON:
Vs Senegal 2-0
Vs Kenya 3-2
Vs Algeria 3-0
Tupe ubuyu huo
ReplyDeleteMuheshimiwa Mwakyembe anaposema bado anaimani na kocha Amunike kwa kigezo gani? Muheshimiwa waziri anaweza kuwa kikwazo kwa maendeleo na ukuaji wa michezo nchini kama ataendelea kuendekeza kuweka siasa mbele kuliko uhalisia wa mambo. Amunike hata raisi wa soka nchini mwake Nigeria anaishangaa Tanzania kumkabidhi timu yetu ya Taifa bila shaka raisi huyo wa chama cha mpira cha Nigeria alijua tu kuwa Amunike atalitia aibu taifa lake kwa kutoa kocha wa hovyo kwenye mashindano hayo ya Afcon. Na ndio maana raisi huyo alisubutu kusema kuwa kama angepata nafasi ya kushauriwa na watanzania kuhusu ajira ya Amunike ndani ya taifa stars yeye angepinga kwani Amunike sio kocha. Ni mambo ya kushangaza sana na kusikitisha kuona waziri akimpamba kocha alieshindwa majukumu yake na asionesha dalili yeyote yakuweza kuleta mabadiliko yeyote ya maana ndani ya taifa stars.Ni Mwakyembe huyo huyo aliewahi kutetea ushiriki wa aibu wa Serengeti boys na kuyaita kuwa yalikuwa mashindano ya mafanikio mpaka muheshimiwa raisi Magufuli alipoamua kuja kutema nyongo na kuamua kuja kusema ukweli. Ila wacha waendelee kumpamba lakini kwa Amunike huyu kama ataendelea kuifundisha Taifa stars basi tutarajie majanga zaidi huko twendako.
ReplyDeleteKwanza nchi yoyote ile ukiona viongozi wa kisiasa wameanza kuingiza mikono yao ktk technical bench la timu ya Taifa ujue tayari mfumo wa mpira wa Taifa hilo una kasoro.
ReplyDeleteSuala la kocha wa Stars wanatakiwa waachiwe TFF na technical director wao waamue kama anawafaa au lkn sio wanasiasa waanze kufanya uharibifu wa wazi kutetea wasichokijua.
Nchi au timu yoyote ile kocha akianza kuleta malumbano na wachezaji huwa anafukuzwa fasta ili kurudisha morali ya wachezaji. Kocha kama hapendwi na wachezaji hamuwezi kufanya vizuri kwenye mashindano.