Na Saleh Ally
MICHUANO ya Kombe la Kagame imemalizika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam huku kukiwa na mengi ya kufurahia na kujifunza.
Ingawa Yanga ndiyo ilipewa nafasi zaidi, safari yake ikaishia robo fainali
na Azam FC ikasonga hadi kukutana na Gor Mahia ya Kenya ambayo imebeba kombe
hilo mara tano tangu ikijulikana kama Luo Union au Luo Star.
Hongera kwa Azam FC kwa kuiwakilisha vyema Tanzania, wachezaji wake,
makocha, viongozi wamefanya kazi yao. Wanastahili pongezi, lakini pongezi zaidi
ni kwa wamiliki ambao wamebadilisha mambo mengi ambayo huenda yalionekana
yasingewezekana hapo awali.
Si rahisi kutaka kufikia mafanikio angalau robo ya yale ya Real Madrid,
Barcelona au Manchester United wakati ndoto zitaendelea kubaki zilezile za
kuamini ‘komandoo’ ndiye mwenye nguvu hata kuliko mwenyekiti wa timu.
Timu kubwa za Ulaya au hata zile kubwa na maarufu za Afrika kama Al Ahly,
Zamalek au TP Mazembe hazikufikia hapo kwa ndoto, yaani wahusika wakiwa
wamelala tu na mambo yakaenda.
Wakati kila kitu cha Azam FC kikienda, tena ikiwa haijafungwa hata bao moja
hadi inafika fainali, gumzo kubwa lilikuwa ni beki Serge Pascal Wawa raia wa
Ivory Coast.
Wawa amekuwa gumzo, Kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee amefikia kumfananisha na
mwanajeshi. Akieleza kama asingecheza soka, basi angekuwa ni mwanajeshi.
Kweli, Wawa amecheza vizuri sana michuano hiyo na amekuwa kiongozi wa
wenzake uwanjani kuhakikisha kila kitu kinaenda bomba. Alikuwa shujaa hadi
mwisho wa michuano.
Uchezaji wa Wawa, umezua maswali na Watanzania wapenda soka wameanza kuhoji
hivi; “Kama kweli Wawa ndiyo hana nafasi kwenye timu ya Ivory Coast, kwa uwezo
wake, basi lazima tujipange maana Tanzania hapa angekuwa tegemeo.”
Si swali baya kujiuliza ingawa kwa kuwa wachezaji wetu wengi wamekuwa
wakishuka viwango na kuwafanya wale wa zamani wabaki kuwa bora zaidi.
Kwa mimi niliyebahatika kumuona Salum Kabunda ‘Ninja’ au Bakari Malima
‘Jembe Ulaya’, Mustapha Hoza, hakika sioni kinachonishangaza kwa Wawa badala
yake nitasifia kweli ni mchezaji mzuri.
Wawa si mchezaji ambaye Tanzania haijawahi kuwa naye katika safu ya ulinzi.
Ni mchezaji ambaye si mzuri kuliko wote ambao Tanzania imewahi kuwa nao. Lakini
ninakubali wengi wa wachezaji wa sasa wanaweza wasiwe na kiwango chake na sasa
ndiyo wakati wa kujipima na kuangalia walipo ndiyo mwisho.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ni kati ya mabeki bora kabisa ambao tumekuwa nao,
bado nampa nafasi ya mmoja wa mabeki bora ambao wana uwezo wa kuongoza wenzao,
wanajituma na wanapambana kwa ajili ya timu, wako tayari kwa lolote.
Wawa anaweza asiwe na ubora wa kutisha, lakini moyo wa kutaka kushinda,
kutokukubali kushindwa, kupambana kwa ajili ya klabu yake na maisha yake ndiyo
jambo linalomfanya aonekane bora kweli.
Usisahau kabla ya kutua Azam FC ametokea katika moja timu kubwa barani
Afrika ya El Merrekh ya Sudan. Si mtu anayebahatisha lakini anapigana kweli kwa
ajili ya mafanikio na inakuwa si rahisi hata akiomba kuongezewa mshahara katika
mkataba mpya, mwajiri akasema hapana.
Wachezaji wetu wanalewa sifa mapema, waoga wasiokubali changamoto, wanaohofia
kutoka nje ya nchi yao. Wanalewa sifa za nyumbani na kujiona wamefika mapema.
Lakini wakijituma kweli na kwa malengo, basi aina ya Wawa wako rundo hadi
watamwagikia.
Wawa hana nafasi kwenye kikosi cha Ivory Coast kwa kuwa yeye ni kati ya
wachezaji 500,000 wa nchi yake wanaojituma, wanaotaka kushinda kitimu na
kufanikiwa kimaisha.
Ushindani uko juu, Wawa anaujua, ndiyo maana anapambana. Hapa nyumbani,
wachezaji wanaamini kuwa Yanga au Simba ndicho kigezo cha kucheza timu ya
taifa. Mgeuzeni Wawa awe ubao, chaki mkononi mwenu, mpige hesabu, majibu
mtabaki nayo wenyewe.
0 COMMENTS:
Post a Comment