October 12, 2015


Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga SC, Yusuph Manji, jana aliendelea na mikutano yake ya kampeni kwa ajili ya kuwania kiti cha Udiwani Kata ya Mabagala Kuu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Katika mkutano huo ambao ulijaza umati kwenye Viwanja vya Mbagala-Zakhem jijini Dar es Salaam, Manji aliongelea masuala mengi ya kuboresha katika kata hiyo likiwemo suala la afya, elimu, ajira, ujenzi, miundombinu na mambo mengine mengi.

“Natambua Mbagala ina hospitali tatu lakini ndani ya mwaka mmoja nitahakikisha kunakuwa na hospitali 20, lakini pia ndani ya muda huo nitahakikisha kunakuwa na kisima kirefu kwa ajili ya kuondoa adha ya maji.

“Nitashughulikia suala la ajira za vijana kwa kujenga masoko kupitia kampuni zangu, masuala ya mikopo kwa akina mama nitayatatua, nitahakikisha tunakuwa na barabara zetu za ndani, kingine ni elimu, nitahakikisha Shule ya Sekondari Mbagala Kuu inakuwa ya kimataifa na kuondoka na changamoto kubwa zinazoikabili kwa sasa,” alisema Manji.

Manji pia alizungumzia suala la kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano kuzungumza naye kuhusiana na kuihamisha kambi ya jeshi iliyo Mbagala ili wananchi wapate nafasi ya kupata makazi na yeye atajenga nyumba za bei nafuu.

"Kampuni yangu itajenga ghala la jeshi kwa namna wanavyotaka katika eneo lolote lile mbali na makazi ya watu, halafu mimi nitafanya kazi ya kujenga nyumba za bei nafuu na kuwahamisha wananchi ambao wanaoishi mabondeni ambayo ni maeneo hatarishi," alisema Manji.

Mkutano huo ulihudhuriwa na idadi kubwa sana ya watu ambayo muda wote walikuwa wakimshangilia. Wengi walifurahishwa na sera zake na wengine wakishangazwa na kumsikia akizungumza kwa lugha ya Kiswahili kinachoeleweka wakati awali taarifa zilienea kwamba Manji asingeweza kuzungumza Kiswahili fasaha.

Kingine kilichowashangaza wakazi hao wa Mbagala ni Manji kuwaeleza ndiyo amefikisha miaka 39, huku wengi wakiwa wanaamini huenda ana miaka angalau 45 au 50.

Kabla ya hapo, Manji alikuwa akifanya kampeni kimyakimya katika mitaa mbalimbali ya Mbagala Kuu akitaka pia kujua matatizo yanayowakabiri wananchi anaowataka kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic