April 25, 2016


Na Saleh Ally, aliyekuwa La Coruna
SAFARI ya kwenda Hispania kuliwakilisha Gazeti la Championi ilikuwa ni sehemu ya mafunzo makubwa katika kazi ya uandishi wa habari ambayo inataka mhusika ujifunze kwa wakubwa na wadogo, kila kukicha.

Nilisafiri pamoja na washindi wa “Kwea Pipa Kwenda Hispania na Azam Sports HD”. Ilikuwa ni safari zaidi ya shule ambayo katika mengi niliyojifunza, machache naona yanaanza kwenda kama nilivyoamini.

Kama nilivyoeleza juzi Jumamosi, kwamba mimi na wenzangu kutoka Tanzania pamoja na washindi wengine na waandishi kutoka Hong Kong na Sweden, tulipewa nafasi ya kukaa karibu kabisa wakati wachezaji wa Deportivo La Coruna wakiingia vyumbani. Lakini mwisho tukapewa nafasi kama hiyo kukaa kwenye Mix Zone.
Mix Zone ni sehemu maalum ya waandishi ambayo wanaweza kuwahoji wachezaji kabla au baada ya mechi. Pale mwandishi anachagua mchezaji anayemhitaji na kumuuliza swali analotaka.
Huu ni utaratibu wa kimataifa, kwa wale waliobahatika kuripoti mechi kubwa au michuano mikubwa kama Kombe la Dunia wanajua inavyokuwa.

Wakati wachezaji wanaingia vyumbani, kulikuwa na ulinzi mkali na watu wengi waliwekwa hatua takribani 50 upande wa pili wa barabara tofauti na sisi ambao tungeweza hata kupeana nao “tano”.

Wakati wachezaji wakishuka, hata kabla ya kufika pale tulipo, ilikuwa ni rahisi kujua aliyeshuka ni nyota kweli, maana watu walipiga kelele za juu zaidi na baada ya muda ungemuona mchezaji huyo anakuja upande wetu.
Walioongoza kushangiliwa walikuwa ni Iniesta, Lionel Messi halafu Neymar ambaye alibaki ndani ya basi peke yake kwa takriban dakika 5, ndiyo akashuka taratibu kabisa.

Luis Alberto Suarez Diaz, alishangiliwa kwa kiwango cha kati. Lakini ushukaji wake kidogo ulinishangaza, kwani alishuka haraka sana na kukimbia kama mtu ambaye alikuwa akihofia kukamatwa.

Uso wake alionekana kama mtu asiyetaka kuonekana au kuzungumza na mtu. Hakutabasamu kama wachezaji wengine, hakuonyesha urafiki na yeyote na aliwapita wachezaji wenzake waliowahi kuteremka kwenye basi na kuwahi kuingia vyumbani.

SUAREZ AKISAINI JEZI ALIYOPEWA NA SALEH ALLY

Kwa kuwa nilikuwa na baadhi ya waandishi wa Hispania, nilimuuliza mmoja kwamba hiyo ni tabia ya kawaida ya Suarez? Akanijibu:

“Kawaida hapa Hispania, wachezaji hawaruhusiwi kuzungumza kabla ya mechi, hofu ni kwamba unaweza kuwapotezea ‘focus’ (uwezo wa kulenga jambo wanalotaka kulifanya kwa ufanisi).

“Lakini Suarez yuko hivyo, ana hasira na anataka kufunga kila mechi ikiwezekana zaidi ya mabao mawili.

“Ukiwa unataka kumhoji, omba afunge. Kama itakuwa Barcelona imefungwa au hajafunga, usimsogelee kabisa, huwa hazungumzi na mara nyingi anakuwa wa kwanza kupanda kwenye basi.”

Hakuendelea kunipa maelezo kwa kuwa tulitakiwa kuondoka eneo hilo na kwenda kupiga picha na wachezaji wa Deportivo La Coruna waliokuwa benchi. Kwa upande wa wachezaji wa Barcelona, tulielezwa kwamba lilikuwa jambo gumu. Hivyo tukafanya hivyo.



Niliangalia mechi nikiwa makini na mambo mengi, lakini maelezo ya Suarez yalinifanya niwe makini sana kwake kwa muda wote wa mechi nikitaka kujua atafanya nini. Alikuwa ndiye mwiba kwa walinzi wa Deportivo La Coruna, akafunga mabao manne, Barcelona ikishinda kwa mabao 8-0.

Wakati wachezaji wanatoka tukiwa katika Mix Zone, nilisubiri atokee Suarez kuthibitisha yale maelezo ya mwandishi kutoka gazeti namba moja la michezo Hispania la Marca.


Alipotoka tu, nilikuwa mtu wa kwanza kumuita. Alitoa ushirikiano kwa kusaini jezi yangu na kujibu swali nililomuuliza. Hakika alionekana ni mwenye furaha, alipiga picha na watoto wawili, halafu akasogea na kupiga picha na mtu mmoja ambaye alimuomba, nikaamini hilo.

Lakini njaa ya Suarez ikaanza kubadili mawazo yangu, kwamba hata Barcelona wenyewe hawaoni kwa kuwa staa mkubwa au tegemeo zaidi kwao ni Suarez, tena kwa sasa anazidi hata umuhimu wa Neymar na Messi.

Utaona baada ya mechi hiyo, iliyofuatia niliishuhudia kwenye runinga, Barcelona wakiwa nyumbani Camp Nou, wakaigaragaza Sporting Gijon kwa mabao 6-0, Suarez akapiga mengine manne, safari hii akiwa na mawili ya penalti.

Suarez ana njaa kweli na ukiangalia, uwanjani utaona ana tofauti kubwa. Kikubwa kinachomsaidia hachezi kama supastaa. Anakimbiza mpira, anakaba, anabugudhi na anapambana muda wote, jambo ambalo ni nadra kumuona Messi, Neymar au hata Cristiano Ronaldo akifanya hivyo.


Ndani ya mechi mbili, kafunga mabao 8. Sasa ndiye anaongoza kwa ufungaji. Kabla ya mechi hizo mbili alikuwa anazidiwa na Ronaldo mabao matano. Sasa anamzidi mshambuliaji huyo nyota wa Real Madrid mabao matatu. Yeye kapiga 34 na Mreno huyo 31.

Awali ilionekana ni vita ya Messi na Ronaldo, sasa Suarez kaingia katikati na huenda akawa ndiye staa namba moja kuliko wote na huenda baada ya msimu huu akawa ndiye gumzo kuliko wote kama alivyoondoka England akiwa tegemeo na gumzo kuliko wote.

Awali ukizungumzia mabao na pasi, ungemtaja Messi. Lakini Suarez anadhihirisha anajua mno mpira na ndiye baba mpya mwenye nyumba wa Barcelona, yaani tegemeo, kwani baada ya kucheza dakika 2880 za La Liga, kafunga mabao 34 akiwa ametoa pasi 15 zilizozaa mabao. Kama hiyo haitoishi, katika dakika hizo amepiga mashuti 115 na 62 yamelenga lango.

Utaona takwimu zake ziko juu hata kuliko Ronaldo aliyecheza dakika 3059, akafunga mabao 31 na kutoa pasi 11 tu za mabao.

Messi naye amecheza dakika 2458, amefunga mabao 25 na pasi 13 za mabao. Neymar amecheza dakika 2787 na kufunga mabao 23 na pasi 10 zilizozaa mabao.

 Maana yake kama utazungumzia mabao na pasi za mabao au asisti, Suarez hadi sasa ni bora zaidi ya Ronaldo, Messi na Neymar.

Ndiyo anakwenda msimu wa pili wa La Liga, lakini anaonyesha si mtu wa kawaida. Suarez aliyetoka England kama mkosaji, Barcelona wakaonekana kama “wamebugi”, sasa ndiye shujaa mpya wa Blaugrana.


Huyu jamaa, anajua sana. Mbishi, si mwepesi kukubali na anachotaka ni kushinda zaidi ya mara moja, kufunga mabao zaidi ya yanayotegemewa na hii haina ubishi, atakuwa hashikiki na ndiye shujaa mpya wa Barcelona, hasa kama hataharibu na yale mambo yake.

TAKWIMU LA LIGA:
WATANO WANAOONGOZA LA LIGA KWA MABAO:

Luis Suárez
Barcelona
Amecheza dakika 2880  
Mabao 34
Asisti 15 

Cristiano Ronaldo
Real Madrid
Amecheza dakika 3059  
Mabao 31
Asisti 11 

Lionel Messi
Barcelona
Amecheza dakika 2458
Mabao 25
Asisti 13 

Neymar
Barcelona
Amecheza dakika 2787  
Mabao 23
Asisti 10 

Karim Benzema
Real Madrid
Amecheza dakika 1838 
Mabao 23
Asisti 6


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic