Achana na mapokezi ya Yanga, haya ya Simba ni kufuru. Wakiwa safarini kuelekea Songea, mastaa wa Simba walisepa na kijiji, na utitiri wa watu ulikuwa mkubwa kiasi cha kusababisha mtu mmoja afariki dunia.
Timu hiyo, juzi alfajiri ilielekea Songea kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopangwa kuchezwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Majimaji.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, timu hiyo ilipata mapokezi makubwa ikiwa njiani ikielekea Songea ilipokwenda kuvaana na Majimaji.
Mtoa taarifa huyo alisema mapokezi ya timu hiyo yalikuwa makubwa walipofika Tunduru, Songea na kupokelewa na kundi kubwa la mashabiki wanaokadiriwa kufikia watu 10, 000.
“Simba walipata mapokezi makubwa tofauti na ilivyotarajiwa kiukweli, kundi kubwa la mashabiki walijitokeza, wanakadiriwa kufikia 10,000 waliojitokeza kuupokea msafara huo.
"Msafara huo ulikuwa mkubwa na kusababisha ajali ya kifo cha mtu mmoja aliyekuwa akiendesha bodaboda ambaye alifariki dunia akiwa anaupokea msafara," alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa meneja wa timu hiyo, Mussa Mgosi, alikiri kutokea hilo, akisema: “Ni kweli imetokea ajali kubwa tulipofika Tunduru tukiwa tunaelekea Songea na hatukupata idadi ya watu waliofariki, lakini nimesikia ni watu wanne tu.”
Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Zuberi Mwombeji, alisema: "Ni kweli Simba walipata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wao waliojitokeza barabarani kuwapokea wakiwa wanaelekea kwenye mechi yao na Majimaji.
"Taarifa ya kifo tuliyoipata ni moja tu kutoka kwa dereva bodaboda aliyefariki muda mchache baada msafara wa Simba kupita eneo hilo ambaye yeye aligonga ukingo wa barabara akiwa spidi na kusababisha afariki dunia."
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment