May 9, 2016


Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi amewataka wachezaji wa timu ya soka ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama jina la Serengeti Boys kwenda kucheza soka la ushindani na kurudi na kikombe nyumbani katika mashindano maalumu ya vijana yatakayofanyika Goa, India.

Dioniz Malinzi aliyasema hayo leo Mei 9, 2016 kwenye hafla ya kukabidhi bendera timu ya Serengeti Boys inayokwenda Goa, India kushiriki mashindano hayo maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF).


Katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam, Dioniz Malinzi alisema: “Msiwe na wasiwasi, wakati wenu wa kucheza soka ndiyo huu.”

“Waziri wa Michezo, Nape Nnauye ameniagiza niwaambie kwamba Serikali itakuwa pamoja nanyi, hivyo msiwe na wasiwasi nendeni mkacheze. Mkacheze mpira wetu si kuigaiga eti mcheze kama Misri. Kachezeni mpira wenu, huu ndio wakati wenu wa kucheza mpira,” aliasa Malinzi.

Wito wa Malinzi ulipokelewa kwa mikono miwili na Nahodha wa timu hiyo, Issa Makamba aliyetamba kurudi na taji hilo mwishoni mwa mwezi mara baada ya mashindano yanayofikia kikomo Mei 26, mwaka huu.

“Tunamshukuru Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwa namna alivyojitahidi kutuhudumia hapa kambini. Tunaahidi tutarudi na kombe hapa,” amesema Makamba na kuongeza kikosi chako kiko vema kama alivyotangulia kusema Mshauri Mkuu wa Maendeleo kwa timu za Taifa, Kim Poulsen.

Naye, Balozi wa India nchini, Sandeep Arya aliyeambatana na Naibu Balozi, Robert Shetkintong balozi amesema amefarijika kuona Tanzania imefanikiwa kupata nafasi hiyo kushiriki michuano hiyo maalumu kwa ajili ya kuiandaa India na fainali zijazo za Kombe la Vijana.

“Tunachofanya kwa sasa ni kukuza ushirikiano kati ya India na Tanzania katika michezo hasa soka. Kama tunavyofahamu soka kwa sasa ni mchezo unapendwa na watu wengi. Unagusa watu wengi na India tumeliona hilo hivyo kwa kuendeleza mchezo na uhusiano ndiyo maana tumekuwa na program za maendelo ya mpira. Tutauendeleza na ninaamini vijana hawa watakuwa chache ya kuuboresha mpira wetu,” amesema.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema kwamba tangu kuanza kwa maendeleo ya soka la vijana, mashindano hayo yamekuwa ni hatua kubwa ya maendeleo ya soka Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa haijawahi kutokea timu kama hiyo ikateuliwa kushiriki michezo ya shirikisho kabla ya fainali za Kombe la Dunia kwa vijana.“Kwa kawaida au tuseme kwa mujibu wa ratiba za fainali kubwa zinazofanyika katika nchi fulani, mwaka mmoja kabla huandaliwa mashindano ya shirikisho kama haya. India mwakani wana mashindano makubwa, fainali za Kombe la Dunia kwa timu za vijana na hivyo ni wameandaa mashindano ya shirikisho ambayo Tanzania, Malaysia, Korea Kusini, Marekani na India wenyewe tumealiwa,” amesema na kuongeza kuwa Serengeti Boys inatarajiwa kusafiri kwenda India Jumatano Mei 11, mwaka huu.

Wachezaji wanaoondoka ni Ramadhan Kabwili, Kelvin Kayego, Samwel Brazio, Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel Mwenda, Nickson Job, Ally Msengi, Issa Makamba, Maulid Lembe, Ally Ng'anzi, Asad Juma, Kelvin Naftari, Yasin Mohamed, Syprian Mwetesigwa, Aman Maziku, Rashid Chambo, Enrick Nkosi, Yohana Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na Muhsin Mkame.

Maofisa watakaosafiri na timu hiyo ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Ayoub Nyenzi, Mshauri wa ufundi wa timu za vijana, Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime, Kocha wa Makipa Mohamed Muharami, Daktari wa timu, Shecky Mngazija na mtunza vifaa Edward Edward.

Michuano hiyo itakayopigwa kwa mfumo wa ligi kwa timu tano kucheza mechi nne, inatarajiwa kuanza Alhamisi Mei 12, 2016 na kwamba AIFF kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.

Tayari Serengeti Boys imecheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa mpaka sasa, mmoja dhidi ya Burundi na miwili dhidi ya timu ya vijana wa Misri (The Pharaohs) na kupata matokeo mazuri na tangu Aprili, 2016 iliweka kambi katika hosteli za TFF zilizopo Karume kujiandaa na michuano hiyo chini ya Shime, akisaidiwa na Sebastian Mkomwa.

Ratiba:
Ratiba ya michuano inaonyesha kwamba Tanzania itafungua dimba na Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia Mei 15, mwaka huu.
Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malysia Mei 21.

Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utchezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa.

Maana ya mashindano:

Kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo maalumu ya vijana kimataifa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Serengeti Boys, kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za vijana barani Afrika dhidi ya Shelisheli Juni 25 hadi Julai 2, 2016.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic