May 20, 2016



Uongozi wa Yanga umesema upo tayari kuwasaidia watani wao, Simba kuwalipia deni la shilingi milioni 70 ili kuwaepusha wasishushwe daraja na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Kauli hiyo imekuja siku chache tangu Fifa kuiagiza Simba kumlipa beki wao wa zamani Mkenya, Donald Mosoti shilingi milioni 70 ndani ya mwezi na kama ikishindwa, basi timu hiyo itakumbana na adhabu kadhaa ambazo zinaweza kusababisha washushwe daraja.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amesema tayari wamewapa taarifa hizo Simba na wanachosubiria ni barua rasmi kabla ya kulipa fedha hizo.

“Ujue Simba ni watani wetu wa jadi, hivyo hatutaki kuona ikishushwa daraja na Fifa, hivyo tunachotaka ni kuona tukiwa nao pamoja kwenye msimu ujao wa ligi kuu.

“Kwa sababu watani wetu hao wana pointi zetu sita kama walizotupa msimu huu, hivyo kama wakishushwa daraja tutazikosa pointi hizo ambazo ni muhimu, zimetusaidia kuchukua ubingwa msimu huu.

“Tulikuwa tuna uwezo wa kuwapa hizo za ubingwa wa ligi kuu tulizozichukua ambazo ni shilingi milioni 70, lakini kutokana na fedha hizo kutakiwa kulipwa kwa dola, tutawasiliana na Caf ili wazihamishe fedha hizo shilingi milioni 70 na kwenda Fifa zitakazokwenda kulipia deni hilo.


“Nafikiri mnafahamu sisi baada ya kufuzu hatua hii ya makundi ya Nane Bora, Caf itatupa shilingi milioni 800 ambazo zipo, hivyo tumeona ni bora tukawasaidia watani wenzetu,” alisema Muro.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic