September 26, 2016



Na Saleh Ally
NAFIKIRI utakuwa umesikia kwamba mabingwa wa Afrika Mashariki, Kilimanjaro Queens wamekuwa wakihaha kupata posho zao.

Wikiendi walishinda kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakisubiri kupewa fedha zao za posho wakati wakiwa Uganda.

Walitakiwa kupewa dola 160 (zaidi ya Sh 341,000) kila mmoja, lakini mambo yakawa magumu na mwisho wakaambulia dola 60 (zaidi ya Sh 128,000), kila mmoja huku wakipewa ahadi ya kumaliziwa.

Ninajua, TFF itakuwa na majukumu mengi lakini lazima ijue inapofikia suala la ahadi basi ni lazima litekelezwe kwa kuwa Kilimanjaro Queens wamefanya jambo ambalo linapaswa kuwa mfano.

Wamebeba ubingwa wa Kombe la Chalenji kwa wanawake kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati likiwa ndiyo linafanyika kwa mara ya kwanza. Tena waliondoka nchini kwa basi, kutokana na ubingwa wakarejea kwa ndege.

Unaona ni watu waliokuwa na moyo wa kufanya vema, kweli walitaka kushinda kwa ajili ya taifa lao. Kwa kuwa hata posho katika mechi za mwisho hawakupewa lakini bado hakukuwa na mgomo.

Maana yake mechi za mwisho kama nusu fainali na fainali ambazo ni ngumu, wao walipambana bila ya kuwa na kitu. Wakaonyesha uzalendo na kupambana vilivyo kwa ajili ya taifa lao.

Tayari wameonyesha uzalendo, wameonyesha ni wale wanaojali na wanataka kupambana na kuleta heshima. Suala la fedha waliliweka kando wakaamua kupigania ambacho hauwezi kukwepa kukiita ni uzalendo.

Safari hii wana haki ya kujisikia vibaya, kwa kuwa walionyesha uvumilivu na wakafanya kazi. Sasa uvumilivu wao usitumike vibaya na kuonekana kama ni sehemu ya kuendelea kuwazungusha. Walipwe fedha zao kwanza za posho, ndiyo masuala mengine yakiwemo ya ahadi yafuatie.

Nimeanza na kukumbusha kuhusiana na fedha zao, hii ni kutokana na tukio hilo la wikiendi ambalo niende moja kwa moja kwamba sikufurahishwa nalo.

Niwaase kina dada wote waliolipigania taifa, kwamba wasikate tamaa na bado pia wanatakiwa kuendelea kupambana kwa ajili ya kuendeleza soka la wanawake ambalo linaweza kujenga sifa na mafanikio zaidi kwa soka letu.

Masuala kama hayo ya TFF, ni majaribu, yanapita pia ni sehemu kama mitihani, lakini msisitizo kwa viongozi wa shirikisho hilo, wakubali kuambiwa na walifanyie kazi hilo wasije wakawakatisha tamaa hata hao wanaojituma.

Pia ninataka kusisitiza kuhusiana na wale ambao walianza kuusaidia mpira wa wanawake, leo unaonekana una matunda, basi wasisahaulike.

Kama TFF iliona hawana sababu ya kupongezwa, basi irejee na kuwashirikisha wakati wa uendelezaji wa mchezo huo katika sehemu mbalimbali. TFF haikuwa na juhudi kubwa, imechukua ‘cream’ ya wale ambao walikuwa wameanza kuonekana.

Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (Kifa) na wadau wengine kutoka katika timu za Sayari Queens, Mburahati Queens na nyingine ndiyo wanajua hatua walipiga vipi hatua.

Kama TFF inataka kuuendeleza mchezo huu, basi iendelee kupiga hatua kwa kuwashirikisha na kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Kitu cha mwisho ambacho ninaweza kuwakumbusha TFF ni hiki; ukiangalia kikosi cha Kilimanjaro Queens ambayo ndiyo Twiga Stars, kina wachezaji wengi sana ambao ni wakongwe.

Maana yake, soka la vijana sasa linatakiwa nguvu iwekwe kuanzia kwa vijana zaidi ili kuhakikisha timu zinaendelea kukua na baadaye kuwa imara. Kama hawatakuzwa vijana, basi waliopo sasa wataondoka na sifa zao.


Wengine ambao wamepoteza kama Rwanda, Kenya na Uganda, wao watakuza vijana na baadaye kuutawala ukanda wetu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic