Nahodha wa Simba, Jonas Mkude, ameonyesha ukomavu kwa kusema licha ya timu yake kupoteza mechi mbili mfululizo, bado hawajakata tamaa na nia yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara iko palepale.
Simba ipo kileleni mwa ligi kuu ikiwa na pointi 35 lakini imepoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya African Lyon (bao 1-0) na Prisons kwa mabao 2-1 kabla ya ligi hiyo kusimama.
Katika mechi 15 za ligi, Simba imeshinda 11, imetoka sare mbili na kufungwa mbili, Mkude amesema takwimu hizo haziwezi kuwatoa katika mbio za ubingwa msimu huu.
Kiungo huyo amesema kuwa, kupoteza mechi mbili ni sehemu ya mchezo lakini wameshabaini makosa yao waliyoyafanya na baada ya mapumziko watayafanyia kazi na kurudi tena katika moto wao.
“Tumefungwa kwa sababu huu ni mchezo ambao una matokeo matatu na tumepokea matokeo haya na hatuna budi kukazana kwenye mechi zijazo kuhakikisha kwamba hatupotezi kama ilivyotokea kwenye mechi hizi mbili za mwisho.
“Hatujakata tamaa kutokana na kufungwa kwani ndiyo kwanza vipigo vimetuamsha zaidi na tutajitahidi kupambana kwa kila hali katika mzunguko wa pili tufanye vizuri,” alisema Mkude.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment