Na Saleh Ally
MUULIZE mchezaji yoyote anayekipiga sasa kuhusiana na suala
la ushirikina na bangi kama ni sehemu ya maisha ya soka ya Tanzania, hatakubali
kuelezea kwa kuwa anaona kama atakuwa anatoa siri za ‘familia’.
Jiulize wewe mwenyewe, kwa nini viongozi na wachezaji ambao
wako katika mchezo wa soka katika kipindi hiki hawataki kuelezea kuhusiana na
mambo hayo mawili wakati wanajua ni tatizo na yanawaathiri.
Majibu yanaweza kuwa mengi, lakini jibu la uhakika ni kwamba,
wachezaji na viongozi wengi wa soka wanaabudu ushirikina pamoja na uvutaji wa
bangi, maarufu kama sigara kubwa.
![]() |
| Lunyamila na Saleh Ally |
Waache waabudu, swali la mwisho je, inawasaidia kufikia
mafanikio? Kama inawasaidia wao, Ulaya na kwingine soka ilikopiga hatua
wanatumia ushirikina, au wanavuta bangi ili kucheza vizuri? Jibu litakuwa
hapana! Hakika inashangaza sana.
Kuna matukio mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza hadi kufikia
hata wadau hao au viongozi kwenda kukodisha maiti kwenye hospitali kubwa jijini
Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mambo ya ushirikina ili timu ishinde.
Lakini Tanzania imewahi kuwa na wachezaji hodari wengi ambao
hauwezi kusema walitengenezwa na bangi au ushirikina, lakini walijulikana
kutokana na uwezo wao kama kipaji au mazoezi ya kutosha.
Angalia Edibily Lunyamila, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’,
Hussein Marsha, Athuman China, marehemu Said Mwamba ‘Kizota’ na Ramadhani
Lenny, Sekiloji Chambua, Mohammed Hussein, nahodha wa zamani wa Simba, Selemani
Matola, Mohammed Mwameja.
Wako wengi sana, lakini huwezi kusema uwezo wao ulitokana na
ushirikina au bangi, baadhi yao waliofanya mahojiano na Championi Jumatatu
wamekiri hilo lipo, lakini hawakutaka kwenda ndani zaidi.
“Kweli ni mambo yanayotokea, imekuwa ni kitu cha kawaida na
inatokana na watu kuamini tu. Lakini siamini kama ni msaada, kikubwa ni mazoezi
na kujilinda kiafya. Ingekuwa uchawi ndiyo kila kitu, basi lazima Afrika ndiyo
ingekuwa inatoa mabingwa wa Kombe la Dunia kila wakati,” anasema Matola
aliyeiongoza Simba yenye mafanikio.
“Wakati nacheza, wachezaji wengi waliokuwa wanavuta bangi
walikuwa wale wavivu. Hivyo wanavuta bangi kujipa nguvu, wanadai wanaondoa
uoga. Lakini mimi nilicheza bila ya kuvuta wala ushirikina na sikuwa muoga,”
anasema beki wa zamani wa Yanga na Simba, Malima maarufu kama Jembe Ulaya.
“Ilifikia wakati watu wakaamini navuta kwa kuwa ni jasiri,
lakini mimi naona ujasiri ni asili ya mtu. Halafu nilikuwa najiamini sana
kutokana na kuwa, nilikuwa nafanya sana mazoezini. Ndiyo maana wachezaji wengi
wakienda Ulaya au Uarabuni wanashindwa kutokana na kutokuwa na bangi ya kutosha
huko walipo, hivyo wanacheza chini ya kiwango.”
Matola na Malima ni
kati ya wanasoka wa miaka ya 1990 na 2000 mwanzoni waliofanya vizuri sana
katika maisha yao ya zamani. Lakini kuna vituko ambavyo msomaji unapaswa
kuvijua. Championi Jumatatu lilifanya mahojiano na wachezaji kadhaa wa zamani
ambao wanasimulia.
Mmoja ni beki pembeni wa zamani wa Yanga, yeye anaeleza namna
walivyowahi kukesha usiku kucha wakifanya masuala ya ushirikina klabu kwao.
“Kulikuwa na lawama kati yetu, wachezaji walilalamika
‘kupigana misumari’, suala hilo likafika kwa uongozi na siku chache baadaye
uongozi ukatuita na kusema siku hiyo tutakula na kulala klabuni, jioni wakaja
wazee.
“Wale wazee wakasema usiku wana tambiko wanataka kufanya,
basi tutakubali na kuanzia kama saa moja usiku akaletwa kondoo. Yule kondoo
akawekwa katikati yetu, wakaanza kusoma hadi saa sita usiku. Baada ya hapo
tukamwagiwa maji fulani hivi.
“Dakika chache yule kondoo akafa huku tunaona. Usiku saa saba
tutashuka kule karibu na uwanja, likachimbwa shimo tunashuhudia na yule kondoo
akazikwa. Baada ya hapo tukaanza kumruka na tukaelezwa hilo ndilo tambiko.”
Huyo ni beki huyo wa pembeni wa zamani wa Yanga, lakini
mshambuliaji wa zamani wa Simba naye anakiri hivyo kwamba kweli, bangi na
ushirikina ndiyo rafiki mkubwa wa timu karibu zote zinazoshiriki Ligi Kuu, Ligi
Daraja la kwanza na hata zile za mchangani.
“Sisi tulikuwa tumeweka kambi kule Bamba Beach, makamu
mwenyekiti wakati huo akaja na kuku we mganga, aliagizwa atamchinja wakati
tukipanda kwenye gari na kila mtu amruke. Hivyo kuku akafungwa kamba akalala
pale hotelini.
“Siku iliyofuata, wakati tunakaribia kupanda kwenye gari,
alipotafutwa kuku akakutwa amekufa. Dah ilikuwa mshikemshike lakini mwisho
mechi hiyo ilikuwa dhidi ya Yanga, nakumbuka fainali ya Kombe la Tusker,
tukashinda bao 4-1.”
Wakati mshambuliaji huyo anasimulia, beki mwingine wa kati wa
zamnai wa Simba anasema waliwaji kupelekwa kwa mganga mkoani Mwanza.
“Kuna mdau mmoja wa Mwanza ndiye alikuwa antupokea,
tulipofika tu alitupokea na kusema ameambiwa timu imechezewa, tukachukuliwa na
kupelekwa kwa mganga kijijini sana. Nakumbuka anaitwa Mzee Nyumbani. Kila
mchezaji alikuwa ana godoro lake na usiku akatupeleka kwenye jiwa refu.
“Mfano kama mbao zinazotumika kurukia kwenye swimming pool.
Basi pale wachezaji tukawa tunaserereka nabaadaye akaimba na kuomba mambo yake
lakini siku ya mechi dhidi ya Kahama United mjini Kahama, matokeo yakawa suluhu
na mechi ilikuwa ngumu.”
Achana na huyo, kuna mchezaji mwingine ameomba jina na timu
yake ifichwe gazetini anaeleza yalifanyika mambo ya kishirikina hadi wakatokwa
na machozi.
“Huwezi kuamini, mganga alisoma mambo yake hadi kondoo
akapoteza nguvu. Baadaye akafungwa sanda kama maiti ingawa alikuwa mzima, usiku
huo tukaambiwa kwenda makaburini. Mganga alitaka kaburi jipya, yaani mtu
kazikwa siku ile au siku mbili zilizopita.
“Tulipofika kule, akachimba lile kaburi usawa wa kiuno na
kumzika yule kondoo, pamoja na kufukia tulimsikia akiendelea kulia. Baadhi yetu
wakaanza kutoa machozi, ilikuwa inaumiza sana. Wakati huo mganga alikuwa na
paka wake mweusi amemfunga kama kama vile mbwa.”
Inaonekana kuna mambo mengi sana, lakini jiulize kama vitu
hivi vina msaada katika soka ya Tanzania. Badala yake inaonekana ni miradi ya
wachache ambao hata ikiguswa wanakuwa wakali sana wakihofia riziki zao zinaweza
kutoweka.
Kweli wao wanafaidika, kwani hata wauza bangi wanaingiza
mamilioni kupitia wanasoka kama ilivyo kwa waganga wa kienyeji na mwisho
wachezaji wa Tanzania, safari yao mwisho inakuwa ni Dar es Salaam.









0 COMMENTS:
Post a Comment